Mar 05, 2021 10:34 UTC
  • Kuanza uchunguzi wa ICC wa jinai za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ICC, imeanzisha uchunguzi kuhusu jinai za kivita zilizofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu.

Fatou Bensouda, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ICC, Jumatano, tarehe 3 Machi 2021 alitoa tamko na kutangaza habari ya kuanza uchunguzi wa mahakama hiyo juu ya jinai za kivita zilizofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika vita ulivyovianzisha huko Ghaza mwaka 2014 na pia katika ujenzi wake wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kwenye ardhi unazowapora Wapalestina za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Baytul Muqaddas Mashariki.

Mwanzoni mwa mwezi uliopita wa Februari, Mahakama ya Kimataifa ya ICC ilitangaza kuwa, ina haki kamili ya kufuatilia kesi ya jinai za kivita zilizofanywa na Israel huko Palestina.

Marekani imetangaza upinzani wake mkali kwa hatua ya mahakama ya ICC ya kuanzisha uchunguzi kuhusu jinai za kivita za Wazayuni. Edward "Ned" Price, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani amesema kuwa, amekatishwa tamaa na uamuzi wa Mahakama ya Kiamtaifa ya Jinai ICC wa kufanya uchunguzi kuhusu jinai za kivita za Israel na kwamba serikali ya Joe Biden hivi sasa inachunguza uwezekano wa kuendeleza vikwazo vilivyowekwa na serikali ya Trump dhidi ya Fatou Bensouda na maafisa wengine wa ICC. Amesema, Wapalestina hawajatimiza masharti ya kuwa taifa lenye nchi yao, hivyo hawana haki ya kuwa wanachama wa Mahakama ya Kiamtaifa ya Jinai ICC wala kushiriki katika mahakama hiyo kama serikali na wala kutoa ushauri au kuwasilisha mashtaka ya aina yoyote ile.

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC

 

Naye waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amedai kuwa, hatua hiyo ya ICC eti inaonesha chuki za mahakama hiyo kwa Mayahudi. Hata hivyo Hazim Qassim, Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina "HAMAS ameunga mkono waziwazi uamuzi huo wa ICC na kusema kuwa, uamuzi wa mahakama hiyo wa kuanzisha uchunguzi kuhusu jinai za Wazayuni, ni ushindi mwingine kwa Wapalestina. Amesema, HAMAS inaunga mkono uamuzi huo wa ICC. Nayo Wizara ya Mambo ya Nje wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina imepokea kwa furaha uamuzi wa mahakama ya ICC wa kuanzisha uchunguzi kuhusu jinai za utawala wa Kizayuni huko Ghaza na katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Muhammad Dahlah, wakili Mpalestin na mtaalamu wa sheria wa kimataifa anasema: Kwa hakika hatua hii ya mahakama ya ICC ni jambo zito sana kwa maafisa na viongozi wote wa Israel, iwe maafisa wa kijeshi au viongozi wa kisiasa kwani jinai za kivita zilizofanywa na wahalifu hao dhidi ya Wapalestina ni kubwa sana. Hivyo kufikia hatua hii ya kufuatiliwa jinai zao ndani ya mahakama ya ICC ni sawa na zilizala na tetemeko la ardhi kwao. Kufikia Muisrael kutiwa mbaroni, au kutuhumiwa au hata kuingizwa katika orodha ya watuhumiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ni mabadiliko makubwa ambayo yanakwenda kinyume na misingi yote mikuu ya Israel. Kwa kweli huo ni msiba mkubwa kwa Waisrael.

Maandamano ya walimwengu ya kutaka Wazayuni wapandishwe kizimbani kwa jinai zao dhidi ya Wapalestina

 

Mwaka 2015, Mamlaka ya Ndani ya Palestina ilikubaliwa kuwa mwanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ICC. Hata hivyo Israel si mwanachama wa mahakama hiyo na ilifanya njama kubwa za kujaribu kuonesha kuwa mahakama ya ICC haina haki ya kisheria ya kufuatilia jinai zianazofanywa na Wazayuni. 

Lakini pia, msimamo wa serikali mpya ya Marekani wa kuikingia kifua kikamilifu Israel na kuilaumu mahakama ya ICC kwa kuanzisha uchunguzi kuhusu jinai za Israel ni uthibitisho mwingine kuwa, siasa za kimsingi za Marekani ni kuunga mkono jinai za Wazayuni kwa hali yoyote ile tena bila ya kudadisi. Uungaji mkono huo mkubwa wa Marekani kwa jinai za Wazayuni, umezidi kuwafedhehesha viongozi wa hivi sasa wa nchi hiyo na kufichua uongo wa madai yao ya kupigania haki duniani. Hata hivyo, hamaki hizo za Wazayuni na viongozi wa Marekani haziwazuii walimwengu kuendelea kuilaani Israel na kuchukua hatua dhidi ya jinai zake.

Tags