Mar 06, 2021 02:55 UTC
  • Makamu wa Rais wa Marekani aunga mkono jinai za Israel dhidi ya wananchi wa Palestina

Kamala Harris, Makamu wa Rais wa Marekani amepinga vikali uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) wa kuanza uchunguzi kuhusu jinai za kivita zilizofanywa na Israel dhidi ya wananchi wa Palestina.

Kamala Harris amesema hayo katika mazungumzo yake ya kwanza kwa njia ya simu na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel na kusisitiza kuwa, serikali ya Marekani inapinga uamuzi huo wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Mwendesha Mashtaka wa Makakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ametangaza kuwa, mahakama hiyo imeanza uchunguzi kuhusu jinai za kivita zilizofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina.

Bi Fatou Bensouda, ameleza kwamba, uchunguzi kuhusu jinai za kivita zilizofanywa na Israel dhidi ya watu wa Palestina utakuwa huru na usiopendelea upande wowote.

Kamala Harris, Makamu wa Rais wa Marekani

 

Mwezi uliopita wa Februari Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ilitangaza kuwa inao ustahiki wa kushughulikia jinai za kivita zilizofanywa na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina. 

Taarifa zaidi zinasema kuwa, hatua hiyo ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imewafurahisha sana Wapalestina na kuukasirisha utawala wa Kizayuni wa Israel.

Utawala ghasibu wa Israel unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palstina umekuwa ukitenda jinai kila uchao dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina ambapo umekuwa ukiwaua kinyama hata watoto wadogo ambao hawana hatia yoyote.