Mar 10, 2021 02:49 UTC
  • UAE : Vikwazo vya Marekani vinatatiza Syria kurudi katika Arab League

Waziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ametoa mwito wa kurejeshwa Syria katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League).

Abdullah bin Zayed Al Nahyan, ametoa wito huo mjini Abu Dhabi katika mkutano na waandishi wa habari aliofanya pamoja na mgeni wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergey Lavrov.

Aidha Al Nahyan amesema, vikwazo vya Marekani dhidi ya serikali ya Rais Bashar al Assad vinakwamisha uwezekano wa Syria kurejea kwenye Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na vinatatiza pia juhudi za kikanda za kuutatua mgogoro wa nchi hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Imarati ameongeza kuwa, ni kwa maslahi ya Syria na nchi zingine za Kiarabu nchi hiyo kurejea kwenye Arab League.

Katika mkutano huo wa pamoja na waandishi wa habari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov alisema, nchi yake inaunga mkono kutatuliwa kwa njia za kisiasa migogoro katika nchi za Syria, Libya na Yemen.

Sheikh Abdullah bin Zayed Al Nahyan (kulia) na mgeni wake Sergey Lavrov

Itakumbukwa kuwa wakati mgogoro na vita nchini Syria vilipoanza mwaka 2011, Imarati ilikuwa moja ya nchi za Kiarabu zilizoyaunga mkono makundi ya upinzani na ya kigaidi nchini humo.

Lakini baada ya jeshi la serikali, likishirikiana na vikosi vya kujitolea vya wananchi, kuyakomboa maeneo mengi yaliyokuwa yakikaliwa na makundi ya kigaidi, nchi za Kiarabu zilizoisusia Syria zilibadilisha muelekeo wao na kuanzisha maelewano na serikali ya Damascus iliyosimamishwa uanachama wake katika Arab League.

Mwaka 2018, Imarati ilifungua tena ubalozi wake nchini Syria kwa mara ya kwanza tangu mataifa ya Kiarabu yalipoanzisha mkakati wa kuisusia nchi hiyo kidiplomasia mwaka 2011.../  

Tags