Mar 31, 2021 03:04 UTC
  • Viongozi wa nchi 23 duniani watoa wito wa kubuniwa mkataba wa kimataifa wa kukabiliana na magonjwa

Viongozi wa nchi 23 wakishirikiana na Mkuu wa Baraza la Ulaya Charles Michel na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani Tedros Adhanom wametoa wito wa kubuniwa mkataba wa kimataifa wa kukabilia na magonjwa mlipuko na migogoro ya afya katika siku zijazo baada ya janga la corona kufichuia jinsi dunia ilivyofeli na kugawanyika katika suala la kupampana na maambukizi ya virusi hivyo.

Viongozi hao wametoa wito huo katika makala yao ya pamoja iliyochapishwa kwenye magazeti ya kimataifa.

Awali Mkuu wa Baraza la Ulaya alikuwa ametoa fikra hiyo katika kikao cha viongozi wa nchi za G20 Novemba mwaka jana ili kuhakikisha kwamba, utoaji wa chanjo, dawa na vipimo vya corona unafanyika kwa uadilifu.

Rasimu ya kuanzishwa mkataba huo jana Jumanne iliungwa mkono na viongozi wa nchi mbalimbali wakiwemo viongozi wa Ureno, Romania, Uingereza, Rwanda, Kenya, Ufaransa, Ujerumani, Korea Kusini, Uholanzi, Tunisia, Uhispania na Afrika Kusini.

Viongozi wa nchi 23 zilizounga mkono fikra hiyo wamesisitiza katika makala hiyo kwamba, kutatokea magonjwa ya mlipuko na dharura kubwa ya kiafya, na hakuna nchi au taasisi moja itakayoweza kukabiliana na tishio kama kivyake na peke yake.

Wametilia mkazo kwamba, nchi zote zinapaswa kubuni mkataba mpya wa kimataifa kwa ajili ya kujiandaa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Makala hiyo imesema, lengo kuu la mkataba huo ni kuimarisha uwezo wa dunia wa kusimama imara mbele ya magonjwa ya milipuko katika mustakbali kupitia njia ya kuboresha mfumo wa tahadhari ya mapema, kupeana taarifa na tafiti na vilevile kushirikiana katika uzalishaji na ugavi wa chanjo, dawa na zana za kujikinga.

Viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wamekuwa wakilalamikia vikali ukiritimba na ubaguzi mkubwa unaoshuhudiwa katika ugavi na usambazaji wa chanjo ya corona duniani. Nchi tajiri zinalaumiwa kwa kujilimbikizia chanjo hiyo.     

Tags