Apr 06, 2021 12:22 UTC
  • Kukosoa Guterres ukiritimba na ugavi usio wa kiadilifu wa chanjo ya Corona baina ya mataifa  ya dunia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine tena amekosoa namna chanjo ya corona inavyozalishwa na kugawiwa baina ya nchi mbalimbali duniani.

Antonio Guterres ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kwamba: Juhudi za kimataifa za kukabiliana na janga la Corona kuanzia uzalishaji wa chanjo na usambazaji wake na kuzisaidia nchi zinazostawi haziendi vizuri kama inavyotakiwa. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameandika: Kama mwenendo hatari wa muelekeo wa utaifa katika uzalishaji wa chanjo ya Covid-19 na ukiritimba katika chanjo hiyo unaofanywa na baadhi ya mataifa tajiri utaendelea, hatua za dunia za kukabiliana na virusi hivyo zitachelewa kupata mafanikio. Kuna haja ya kuwa na uhakika kwamba, chanjo ya Corona inapatikana na inawafikia wote na kwa gharama nafuu.

Hii si mara ya kwanza kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kukosoa hilo, kwani huko nyuma pia aliwahi kukosoa namna chanjo ya Corona inavyogawiwa kwa nchi mbalimbali duniani na akasisitiza kwamba, jambo linalopaswa kupewa kipaumbele katika mwaka huu wa 2021 ni watu wote kuweza kupata chanjo ya Corona kwa urahisi.

 

Indhari ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na ukiritimba na mwenendo usio wa kiadilifu na hata wa kujilimbikia chanjo ya Corona inapaswa kupewa umuhimu hasa kwa kutilia maanani utendaji wa hivi sasa wa madola makubwa ya Magharibi hususan Marekani na baadhi ya madola ya Ulaya.

Kimsingi ni kuwa, mataifa haya hususan Marekani ambayo yanadai kuwa mstari wa mbele katika kugundua na kuzalisha chanjo mbalimbali za Corona, badala ya kugawa kwa uadilifu chanjo hizo baina ya mataifa ya dunia, yanachukua hatua za kulimbikiza chanjo hizo na kuzitumia kwa ajili yao tu.

Akizungumza hivi karibuni katika Mkutano wa Usalama wa Munich nchini Ujerumani, Guterres alisema kuwa: Asilimia 75 ya chanjo ya Corona imegawiwa katika nchi 10 tu duniani huku zaidi ya nchi 100 zikisalia bila ya chanjo.  Ni kwa msingi huo, ndio maana Antonio Guterres anataka kuweko mpango wa kimataifa wa kugawa chanjo ya Corona.

Dkt. Ombeva Malande mmoja wa wafanyakzi wa afya nchini Uganda akionesha kadi yake ya chanjo baada ya kupatiwa chanjo dhidi ya COVID-19 katika hospitali ya Mulago jijini Kampala (10/03/2021)

 

Filihali mataifa ya Magharibi kama Canada imejilimbikizia kiwango kikubwa cha chanjo ya Corona bila ya kuzingatia kwamba, kiwango hicho cha chanjo hakiendani na idadi ya watu wa nchi hiyo. Hadi sasa serikali ya Canad imeagizia dozi milioni 400 za chanjo ya Corona, katika hali ambayo idadi ya jamii ya nchi hiyo ni chini ya milioni 40.

Kiujumla na kwa mujibu wa takwimu za mataifa yaliyoendelea na tajiri ni kuwa, mataifa hayo yameagizia dozi za chanjo ya corona ambazo ni mara tatu ya idadi ya watu katika nchi zao hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu (2021). Hali hii inapunguza uwezekano wa mataifa yanayoendelea na yenye kipato kidogo kuweza kupata chanjo hiyo. Kimsingi ni kuwa, kununua mataifa hayo chanjo zaidi ya mahitaji, inazuia ugavi wa usawa wa chanjo hiyo ulimwenguni.

Kwa utaratibu huo, ushindani ulioibuka baina ya mataifa hayo kwa ajili ya kununua chanjo ya Corona, unazinyima fursa ya kupata chanjo hiyo nchi ambazo zimo katika mkondo wa kustawi.

“Muungano wa Wananchi wa Chanjo” ambayo ni moja ya taasisi kubwa kabisa ya kimataifa ya misaada ya kibinadamu Desemba mwaka jana (2020) ilitahadharisha kwamba, yamkini mataifa yenye kipato kidogo yakachukua miaka mingi na yasiweze kupata chanjo hiyo.

Licha ya vikwazo vya Marekani, lakini Iran imeweza kutengeneza chanjo kadhaa za Corona

 

Anna Marriott, mmoja wa maafisa wa shirika la misaada ya kibinadamu la Oxfam anasema: Hakuna mtu anayepaswa kunyimwa fursa ya kupata chanjo ambayo ni mwokozo wa maisha. Kwa nini mtu anyimwe fursa hiyo kwa sababu tu ni masikini au hana fedha za kutosha kwa ajili ya kununua chanjo hiyo?

Jambo jingine katika suala la ugavi wa chanjo ya Corona na vizingiti vya kupata chanjo hiyo linarejea katika kadhia ya vikwazo. Kuendelea vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya mataifa mbali mbali yanayopinga ubeberu wa Washington kama Iran, kimekuwa kizingiti kikubwa cha kupata chanjo hiyo. Serikali ya Joe Biden, licha ya nara zake, lakini imeendelea kutekeleza siasa za mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa dhidi ya Iran katika uga wa dawa na vifaa vya tiba hata katika kipindi hiki cha msambao wa virusi vya Corona duniani.

Tags