Apr 07, 2021 07:42 UTC
  • Russia na Hizbullah zataka kufunguliwa ofisi ya uwakilishi Moscow

Serikali ya Russia na Harakati ya Hizbullah ya Lebanon zinatafakari kuhusu uwezekano wa kufunguliwa ofisi ya uwakilishi ya harakati hiyo ya muqawama katika mji mkuu wa Russia, Moscow.

Hayo yaliripotiwa jana Jumanne na gazeti la al-Khbar la Lebanon ambalo limefafanua kuwa, mwito wa kufunguliwa ofisi hiyo ya Hizbullah jijini Moscow limetolewa kufuatia mkutano wa ngazi ya juu baina ya maafisa wa Hizbullah na Russia mjini Moscow mwezi uliopita wa Machi.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, pande mbili hizo katika mkutano huo wa Moscow zilisisitizia haja ya kuimarishwa njia za mawasiliano ya moja kwa moja baina ya Hizbullah na Russia.

Mbali na wajumbe wa Russia na Hizbullah kujadili uhusiano wa pande mbili katika mkutano huo wa Machi 15, lakini pia waligusia kuhusu hali ya Yemen, Iraq, Syria na Palestina.

Waziri Lavrov wa Russia akiupokea ujumbe wa Hizbullah mjini Moscow Machi 15, 2021

Ujumbe wa Hizbullah katika mkutano huo wa Moscow uliongozwa na Mohammad Raad, Mkuu wa Tawi la Kisiasa la harakati hiyo ya mapambano ya Kiislamu ya Lebanon, huku ujumbe wa Russia ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje ya nchi hiyo, Sergey Lavrov.

Baada ya kujiri mkutano huo mjini Moscow, Ammar Musawi, Afisa wa Mahusiano ya Kigeni wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon alisisitiza kuwa, harakati hiyo imefikia makubaliano na Russia ya kuimarisha ushirikiano baina yao kuhusiana na masuala yote yanayohusu maslahi ya pamoja.

 

Tags