Apr 07, 2021 08:08 UTC
  • Kikao cha Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA mjini Vienna na tetesi za kuondolewa vikwazo

Vienna, mji mkuu wa Austria jana Jumanne ulikuwa mwenyeji wa kikao cha kawaida cha Kamisheni ya Pamoja ya mazungumzo ya nyuklia, JCPOA.

Kabla ya kikao hicho, kikao cha 18 cha Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA kilifanyika Ijumaa iliyopita kwa njia ya video, ambapo washiriki Iran na kundi la 4+1, waliamua kuendeleza kikao hicho ana kwa ana mjini Vienna.

Baada ya kufanyika kikao hicho cha Ijumaa cha Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA, habari zilienea kwamba ujumbe wa Marekani ulikuwa umeamua kufika mjini Vienna siku ya Jumanne kwa ajili ya kufanya mazungumzo na wanachama waliosalia katika mazungumzo ya nyuklia ya JCPOA isipokuwa Iran.

Akitoa radiamali yake kuhusu suala hilo, Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema kuwa kikao cha Jumanne hakikuwa tofauti na vikao vingine vilivyopita vya Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA na kusisitiza kuwa: Njia iko wazi; vikwazo vyote vya Marekani vinapaswa kuondolewa na hilo kuthibitishwa kivitendo. Kuna hatua moja tu nayo ni kuondolewa vikwazo vyote vya Marekani na baada ya hapo Iran itakuwa tayari kusimamisha hatua zake za kufidia hasara na kurejea nyuma.

Abbas Araqchi anayeongoza ujumbe wa Iran katika mazungumzo ya Vienna

Akiashiria madai yaliyotolewa na gazeti la la Wall Street Journal kuhusu kufikiwa mapatano mawili muhimu mjini Vienna, Khatibzadeh amesema: Uamuazi wa kundi la 4+1 kuhusu sehemu na vipi litafanya mazungumzo na Marekani ni suala linalolihusu kundi hilo tu.

Sayyid Abbad Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na amabaye anaongoza ujumbe wa Iran katika mazungumzo ya Vienna pia amesema: Katika mazungumzo ya Vienna ni wanachama wa hivi sasa tu wa JCPOA ndio waliopangiwa kushiriki mazungumzo hayo na wala Marekani haitaruhusiwa kushiriki mazungumzo ambayo Iran inashirikishwa yakiwemo haya ya Kamisheni ya Pamoja, na hilo ni jambo lisilo na shaka yoyote.

Huku akisema kuwa Russia inaheshimu mtazamo wa Iran kuhusu jambo hilo, Sergei Ryabkov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kwamba: Hadi pale Tehran itakapochukua uamuzi tofauti, kwa sasa tunaendelea na mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja, jambo ambalo linakubaliwa na wote ikiwemo Marekani yenyewe.

Msimamo wa Iran kuhusu mapatano ya JCPOA uko wazi na unafungamana moja kwa moja na haki zake katika mapatano hayo. Iran itarejea tu katika utekelezaji wa majukumu yake ya awali katika mapatano ya JCPOA iwapo Marekani itaondoa vikwazo vyote vya kidhalimu ilivyoiwekea. Kwa msingi huo Marekani haina chaguo jingine isipokuwa kuondoa kivitendo vikwazo hivyo vyote, na hilo kuthibitishwa na Iran kwamba kweli vimeondolewa. Kusimamishwa kwa vikwazo vipatavyo 1500 vilivyowekwa na Ofisi ya Udhibiti wa Fedha ya Wizara ya Fedha ya Marekani dhidi ya Iran ni hatua ya msingi inayopaswa kuchukuliwa na Marekani.

Mazungumzo ya Iran na kundi la 4+1 mjini Vienna

Joseph Cirincione, Mwanachama wa Baraza la Uhusiano wa Kigeni la Marekani amesema kuwa bila kujali ni nini kitafikiwa katika mazungumzo ya Vienna, la muhimu ni kuwa mazungumzo hayo yatachukuliwa kuwa na umuhimu pale yatakapopelekea kuchukuliwa hatua muhimu katika kuondoa dhana mbaya, shaka, vizuizi na uingiliaji usiofaa kati ya pande mbili; la sivyo haitawezekana kurejea katika mapatano ya JCPOA.

Kwa vyo vyote vile azma ya kisiasa ndio injini ya juhudi za kuhuishwa mapatano ya JCPOA na kukabiliana na changamoto zilizopo za kiufundi na zisizo za kiufundi katika uwanja huo. Pamoja na hayo na kwa kuzingatia uzoefu wa huko nyuma wa Marekani kukiuka mapatano ya JCPOA, itakuwa vigumu kwa pande mbili kufikia makubaliano ya kuridhisha katika uwanja huo. Jambo lenye umuhimu katika tetesi zinazoenezwa na vyombo vya habari vya Magharibi kuhusu mazungumzo ya Vienna ni utendaji na kurejeshwa imani iliyopotea kutokana na matamshi na vitendo vya Marekani vya kukiuka sheria na ahadi.