Apr 08, 2021 07:26 UTC
  • Zaidi ya wabunge 70 wamtaka Rais wa Marekani akomeshe kuzingirwa Yemen

Zaidi ya wabunge 70 wa Marekani jana walimuandikia barua rais wa nchi hiyo Joe Biden wakimtaka afanye juhudi za kukomeshwa kuzingirwa kidhulma Yemen.

Wajumbe hao wa Baraza la Wawakilishi la Congress ya Marekani aidha wameitaka Saudi Arabia iondoe mzingiro wake wote dhidi ya Yemen kwani umesababisha upungufu mkubwa wa chakula na mafuta katika nchi hiyo maskini ya Kiarabu.

Miongoni mwa waliotia saini barua hiyo ni Adam Schiff, mkuu wa kamati ya taarifa za kijasusi ya Baraza la Wawakilishi la Marekani na Jerrold Nadler, mkuu wa kamati ya mahakama ya bunge hilo.

Maelfu ya watoto wa Yemen wameuliwa kidhulma na muungano wa Saudia

 

Barua hiyo imeandikwa baada ya ripoti ya hivi karibuni ya televisheni ya CNN iliyozungumzia maafa makubwa ya wananchi maskini wa Yemen yaliyosababishwa na mashambulio makubwa ya miaka mingi na kuzingirwa kila upande nchi hiyo ya Kiarabu. Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema kuwa, Yemen ni sehemu yenye mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu hivi sasa.

Saudi Arabia, ikiungwa mkono kwa hali na mali na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Marekani, utawala wa Kizayuni, Uingereza na nchi kadhaa nyingine mwezi kama vile Sudan, mwezi Machi mwaka 2015 ilianzisha mashambulizi ya kijeshi ya pande zote dhidi ya Yemen na kuiwekea mzingiro wa angani, baharini na nchi kavu nchi hiyo maskini ya Kiarabu. 

Hadi sasa Wayemeni zaidi ya elfu 16 wameshauawa katika vita hivyo vya muungano vamizi unaoongozwa na Saudia, huku makumi ya maelfu ya  wakijeruhiwa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.