Apr 08, 2021 07:32 UTC
  • 'Vifo vya corona nchini Brazil ni maafa makubwa kama ya bomu la nyuklia'

Baada ya kuongezeka kupindukia idadi ya watu wanaofariki dunia kila siku kwa COVID-19 nchini Brazil, wataalamu wa afya wa nchi hiyo wamelifananisha janga hilo na maafa ya bomu la nyuklia na wanasema kuwa Brazil sasa hivi imekumbwa na balaa la "Fukushima za Biolojia."

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, wataalamu wa Afya wa Brazil wameonya vikali kuhusu hali ya hatari iliyoikumba nchi hiyo na kusema kuwa, karibuni hivi idadi ya vifo vya corona nchini humo itapindukia ile ya Marekani.

Katika ripoti yake, Waziri wa Afya wa Brazil amesema, idadi ya watu waliofariki dunia nchini humo kutokana na ugonjwa wa corana imeshapindukia laki 3 na 37,000.

Licha ya kuwa na idadi ndogo ya wakazi wake ikilinganishwa na wale wa Marekani yaani takriban thuluthi mbili ya wakazi wa Marekani, lakini sasa hivi Brazil imepishana kidogo tu na Marekani katika idadi ya watu waliofariki dunia kwa COVID-19 na sasa hivi Brazil imekuwa ndicho kitovu cha ugonjwa wa corona duniani.

Maafa ya corona ni makubwa sana Brazil, lakini rais wa nchi hiyo bado anapinga kuchukuliwa hatua za kujikinga nao

 

Wakati ambapo wataalamu wa afya duniani wote wanakubaliana kwamba kuvaa barakoa na kuweka karantini na watu kutokurubiana ndizo njia bora za kujiepusha na ugonjwa huu unaoenea zaidi kupitia watu kupumuliana, lakini Rais Jair Bolsonaro wa Brazil bado anapinga kulazimishwa watu kuheshimu miongozo hiyo ya madaktari. Licha ya maafa makubwa ya corona, lakini viongozi wa ngazi za juu wa Brazil bado wanashikilia kuwa, janga hilo litadhibitiwa haraka nchini humo na mambo yatarejea katika hali yake ya kawaida karibuni hivi.

Moja ya sababu kuu za kuenea vibaya ugonjwa wa corona huko Brazil ni siasa mbovu za rais wa nchi hiyo. Bado Rais Jair Bolsonaro wa Brazil anashikilia kuwa, ugonjwa huo umeletwa na mabeberu na anapinga kuchukuliwa hatua za kiafya za kujikinga nao kama vile karantini na watu kutokurubiana.

Tags