Apr 08, 2021 08:07 UTC
  • Kikao cha pamoja cha JCPOA; matarajio ya kundi la 4+1 na matumaini ya Iran

Kikao cha 18 cha Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA kilifanyika juzi Jumanne huko Vienna mji mkuu wa Austria kwa kuhudhuriwa na wawakilishi wa kundi la 4+1 na pia Iran. Nchi wanachama wa mapatano ya JCPOA baada ya majadiliano na kuchunguza mapatano hayo zimekubaliana kuendeleza mashauriano katika ngazi ya kitaalamu ili kuiondolea Iran vikwazo.

Vikao hivyo vinatazamiwa kufanyika katika fremu ya timu mbili tofauti za watalaamu kuhusu masuala ya kiufundi ya kuondoa vikwazo na kutekeleza kikamilifu mapatano ya JCPOA na kisha kuwasilisha matokeo ya vikao hivyo kwa kamisheni ya pamoja ya JCPOA. 

Timu ya mazungumzo ya Marekani iliyofika Vienna ilifikia katika hoteli moja katika mji huo; lakini haikushiriki katika Kikao hicho cha Pamoja cha Kamisheni ya JCPOA. Iran ilitangaza kuwa haiko tayari kufanya mazungumzo ya pande mbili wala ya pande kadhaa na Marekani. Enrique Mora Naibu Katibu Mkuu wa Idara ya Hatua za Nje ya Umoja wa Ulaya baada ya kumalizika kikao hicho aliyataja mazungumzo ya kwanza kuwa mazuri nakuongeza kuwa "kuna umoja na shauku ya kupatikana mchakato wa pamoja wa kidiplomasia na makundi mawili ya kitaalamu ili kutekeleza mapatano ya nyuklia na kuondoa vikwazo."  

Mikhail Olyanov Mwakilishi wa Russia katika taasisi za kimataifa huko Vienna Austria pia ameeleza haya katika mtandao wake wa Twitter kwamba, mafanikio muhimu zaidi yaliyopatikana katika kikao cha Vienna ni kuanza hatua za kivitendo za kuhuisha mapatano ya JCPOA.  

Mikhail Olyanov, Mwakilishi wa Russia katika taasisi za kimataifa huko Vienna Austria  

Ned Price Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani pia ameyataja mazungumzo ya nyuklia ya Jumanne wiki hii huko Vienna kuwa yenye mafanikio na hatua moja mbele. Ameongeza kuwa, njia pekee waliyojielekeza hivi sasa ni kurejea kwa pande mbili katika mapatano ya nyuklia ya mwaka 2015. Licha ya matarajio hayo, lakini msimamo wa Iran kuhusu kwa namna gani itarejea katika majukumu yake ya JCPOA upo wazi na imara. Kwa hivyo hali ya mambo ya sasa itasalia kama ilivyo hadi hapo Washington itakapoikidhia Tehran matakwa yake. 

Sayyid Araqchi Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Mkuu wa Timu ya Iran katika Kikao cha Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA amesisitiza kuwa, kuondolewa vikwazo vya Marekani ni hatua ya kwanza na dharura zaidi ili kuhuisha mapatano hayo; na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kikamilifu kusitisha hatua zake za ufidiaji na kurejea katika utekelezaji kamili wa mapatano ya JCPOA iwapo vikwazo dhidi yake vitaondolewa na kisha ijiridhishe na jambo hilo. 

Sayyid Araqchi, Mkuu wa Timu ya Iran katika Kikao cha Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA

Serikali ya Trump mwezi Mei mwaka 2018 ilijitoa kwa upande mmoja katika mapatano hayo ya kimataifa na kisha ikitekeleza wenzo wa mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi ili kuwaweka chini ya mashinikizo wananchi wa Iran na kuilazimisha Tehran ikubali matakwa yake yaliyo kinyume cha sheria. 

Mkabala wake Iran imetekeleza siasa za muqawama wa hali ya juu na kufanikiwa kukabiliana pakubwa na mashinikizo hayo ya kiwango cha juu zaidi ya Washington; na serikali ya Trump imeshindwa kufikia hata lengo lake moja. 

Robert Malley Mjumbe Maalumu wa Marekani katika masuala ya Iran amekiri kuwa wenzo wa mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi dhidi ya Iran umefeli. 

Rais Mpya wa Marekani Joe Biden pia hata kama amekosoa siasa za serikali iliyopita ya nchi hiyo kuhusu Iran lakini ameainisha suala la Iran kutekeleza tena majukumu yake ndani ya JCPOA kama sharti la Marekani kurejea katika mapatano hayo.

Rais Joe Biden wa Marekani 

Aidha bila ya kuashiria ni nchi ipi iliyokwenda kinyume na kujitoa katika mapatano ya JCPOA, Biden ameahidi kuwa kama Iran itarejea kutekeleza majukumu yake ndani ya mapatano JCPOA Washington pia itarejea katika mapatano hayo.  

"Imad Abshanas mchambuzi wa masuala ya kisiasa anasema: serikali ya Biden haina siasa za wazi kuhusu mapatano ya JCPOA; na kuna ukinzani wa hali ya juu ndani ya serikali ya Marekani kuhusu suala hilo. Baadhi ndani ya Marekani wanataka kutumia vibaya suala la vikwazo dhidi ya Iran vilivyowekwa na serikali ya Trump na wengine wanaamini kwamba vikwazo hivyo havikuwa na tija na Marekani inapasa kurejea katika mapatano ya JCPOA." 

Nchi wanachama wa Ulaya wa kundi la 4+1 ambazo sasa zinaratibu misimamo yao na serikali ya Biden huko nyuma zilipendekeza kufanyika kikao kisicho rasmi kati ya wanachama wa mapatano ya JCPOA na Marekani; pendekezo ambalo limepingwa na Tehran. Katika wakati huu nyeti, Iran imetangaza kuwa Marekani haitashiriki katika kikao chochote ambacho Iran itahudhuria hadi itakapoonda vikwazo vyake na jambo hilo kuthibitishwa. Kwa hiyo jitihada zinazofanywa na Marekani kwa ajili ya kushiriki huko Vienne sambamba na Kikao cha Pamoja cha Kamisheni ya JCPOA kwa lengo la kuanza mazungumzo na Iran zimegonga mwamba. 

Tags