Apr 11, 2021 03:36 UTC
  • Dunia yaendelea kukosoa azimio la Seneti ya Ufaransa kuhusu marufuku ya hijabu

Watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Ufaransa na maeneo mengine ya dunia wameanzisha kampeni iliyopewa jina la Hands Off My Hijab (@handsoffmyhijab) wakieleza hasira zao dhidi ya azimio la Baraza la Seneti la Ufaransa la kuzidisha vizuizi na marufuku dhidi ya vazi la staha la mwanamke wa Kiislamu, Hijabu. Watu wengi wamesema kuwa azimio hilo linapiga vita Uislamu. 

Wimbi la upinzani wa ndani na nje ya Ufaransa dhidi ya hatua hiyo lilianza baada ya kuwasilishwa muswada wa azimio hilo katika Seneti ya Ufaransa. Wakati huo kundi la wanawake Waislamu wa Ufaransa lilianzisha harakati ya kupinga hatua hiyo na kufuatiwa na makundi ya wasomi na baadhi ya vinara na viongozi wa kidini. Baadaye wimbi hilo lilishika kasi zaidi na kusambaa baina ya watumiaji wa mitandao ya kijamii ambao wamelaani hatua ya serikali ya Emmanuel Macron wa Ufaransa ya kuzidisha mbinyo na mashinikizo dhidi ya Waislamu.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kuwait, Abdullah Al-Shayeji anasema: Kushadidi unyama na uadui wa usekulari nchini Ufaransa dhidi ya Uislamu umezidisha misimamo ya kufurutu ada ya Emmanuel Macron mkabala wa Marine Le Pen, kiongozi wa wafuasi wa mrengo wenye misimamo mikali wa mrengo wa kulia, kwa ajili ya kinyang'anyiro cha uchaguzi ujao wa rais. 

Emmanuel Macron na Marine Le Pen 

Hivi karibuni Baraza la Seneti la Ufaransa lilipasisha marufuku ya vazi la Hijabu kwa wasichana wa Kiislamu wenye umri wa chini ya miaka 18. Baraza hilo pia limezidisha kifungu kingine katika azimio hilo amacho kinapiga marufuku kutekeleza ibada na desturi za kidini katika vyuo vikuu vya Ufaransa. Azimio hilo lililopasishwa tarehe 30 Machi mwaka huu ni sehemu ya sheria pana iliyopewa jina la "Mapambano dhidi ya Utengano". Muswada wa zimio hilo ulipendekezwa mwaka jana na Rais Emmanuel Macron na limekosolewa sana ndani ya nje ya nchi hiyo kutokana na kuwabana na kuwakandamiza Waislamu.

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, sababu ya hatua hiyo ya Seneti ya Ufaransa inayodhibitiwa na wahafidhina ni kukaribia kipindi cha uchaguzi wa rais na jitihada za mrengo wa kulia-kati za kutaka kupata kura nyingi za wananchi kupitia njia ya kuzidisha mbinyo na chuki dhidi ya Waislamu (Islamophobia) na kuchochea chuki na uhasama dhidi ya raia wa kigeni (Xenophobia).

Islamophobia na mwenendo wa kuchochea chuki dhidi ya Waislamu umeshika kasi zaidi nchini Ufaransa katika miaka ya karibuni. Mwenendo huo sasa umechukua mkondo mpana na hatari zaidi baada ya mabunge ya Ufaransa kuunga mkono misimamo inayopiga vita Uislamu ya Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo. Msingi wa mitazamo hiyo ya Macron ni usekulari uliochupa mipaka unaotaka kuwepo mapambano dhidi ya dini na mafundisho yake katika jamii. 

Wakosoaji wa azimio linalopiga vita Uislamu la Seneti ya Ufaransa wanasema kuwa, Emmanuel Macron anataka kutumia suala hilo kwa malengo ya kisiasa. Hassan Qutamesh ambaye ni mwanaharakati katika mitandao ya kijamii anasema: "Vita ya hijabu nchini Ufaransa ni jitihada za Macron za kujitengeneza ushindi bandia baada ya serikali yake kufeli katika mambo mengi; na katika upande mwingine ni vita ya wazi dhidi ya Uislamu na utambulisho wake." 

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa

Raia wa Ufaransa hususan Waislamu, wamekuwa wakifanya maandamano mara kwa mara na kutahadharisha kuwa, azimio la Seneti ya nchi hiyo litabana uhuru wa kidini na kuwafanya Waislamu wote kuwa washukiwa wa uhalifu. 

Hii ni katika hali ambayo kwa sasa Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amezidisha misimamo yake isiyo ya kimantiki ya kuunga mkono kwa pande zote harakati zinazopinga Uislamu na kuvunjia heshima matukufu ya dini hiyo.        

Tags