Apr 12, 2021 02:46 UTC
  • New York Times: Mashinikizo ya kiwango cha juu dhidi ya Iran yamefeli

Gazeti la New York Times la Marekani limeandika kuwa, uhakika mchungu ni kwamba mashinikizo ya kiwango cha juu dhidi ya Iran yamefeli na kushindwa.

Baraza la Wahariri wa gazeti la New York Times limeandika katika makala hiyo iliyopewa jina la "Kufeli Mashinikizo ya Kiwango cha Juu dhidi ya Iran", kwamba kurejea Marekani katika makubaliano ya nyuklia itakuwa hatua ya awali ya kuondoka katika kinamasi hicho.

Gazeti hilo limeongeza kuwa, Marekani na Iran zimebakia na fursa ndogo ya kurejea katika utekelezaji wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. New York Times limeongeza kuwa, kwa sasa misimamo mikali haioani na akili timamu na kwamba, iwapo Marekani haikuheshimu na kutekeleza makubaliano awali kwa nini Iran iwe na imani na makubaliano mengine ya pili?

Baraza la Wahariri wa New York Times limesema kuwa, uhakika mchungu ni kwamba, mashinikizo ya kiwango cha juu hayakuweza kubadili mienendo ya Iran bali kinyume chake, Tehran iliiadhibu Marekani kwa kusitisha utekelezaji wa baadhi ya vipengee vya makubaliano hayo ya nyuklia kwa sababu ya Washington kujiondoa katika makubaliano hayo, na kuifundisha Marekani jinsi dunia inavyokuwa bila ya makubaliano ya JCPOA.

Mwishoni mwa makala hiyo Baraza la Wahariri wa New Yok Times limetahadhadisha kuwa, iwapo makubaliano ya nyuklia ya JCPOA hayatahuishwa, mwezi Mei mwaka huu wakaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia hawatakuwa na uwezo wa kukagua yanayofanyika katika vituo vya kuzalisha nishati ya nyuklia nchini Iran. 

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, Troika ya Ulaya haikutekeleza ahadi na majukumu yake ya kufidia athari mbaya zilizosababishwa na kujiondoa Marekani katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA hapo mwaka 2018 licha ya kupinga kwa maneno matupu hatua hiyo ya serikali ya Washington. 
Ikijibu hatua ya nchi za Magharibi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilisitisha utekelezaji wa baadhi ya vipengee vya makubaliano hayo, na hivi karibuni ilisimamisha kabisa utekelezaji wa kujitolea wa protokali ziada ya wakala wa IAEA.