Apr 12, 2021 08:08 UTC
  • Jeshi la Myanmar linazitoza dola 85 familia ili kupatiwa miili ya ndugu zao waliouawa na jeshi

Wanaharakati wa haki za binadamu nchini Myanmar wanasema kuwa, kila familia inayotaka mwili wa ndugu yao aliyeuawa na vikosi vya usalama katika ukandamizaji wa Ijumaa iliyopita inalazimika kutoa dola 85 za Kimarekani.

Ripoti za wanaharakati hao zinasema kuwa, jeshi limekuwa likizitoza familia kiwango hicho cha dola 85 za Kimarekani ili zipatiwe miili ya ndugu zao kwa ajili ya kwenda kuzika.

Hatua hiyo ya jeshi la Myanmar ya kukataa kutoa miili hiyo ila baada ya familia husika kulipa gharama ya dola 85 imelalamikiwa mno na wanaharakati wa haki za binadamu nchini humo.

Kwa akali raia 82 waliuawa Ijumaa iliyopita huko Bago yapata kilimota 90  kaskazini mwa mji wa Yangon baada ya vikosi vya usalama kuuvamia mji huo kwa ajili ya kuwatawanya waandamaji waliokuwa wakilalamikia hatua ya jeshi ya kutwaa kwa nguvu madaraka ya nchi. "Ni kama mauaji ya kimbari", alisikika mmoja wa mashuhuda wa mauaji hayo.

Maandamano ya wananchi wa Myanmar ya kupinga mapinduzi ya kijeshi

 

Jeshi la Myanmar lilitwaa madaraka ya nchi Februari Mosi mwaka huu baada ya kumkamata Rais wa nchi hiyo, Win Myint na viongozi wengine akiwemo Aung San Suu Kyi, kiongozi wa chama tawala mwenye ushawishi mkubwa, kufuatia siku kadhaa za mivutano nchini humo.

Kisingizio cha jeshi cha kufanya mapinduzi hayo ni madai yake ya kutokea wizi na udanganyifu katika zoezi la uchaguzi wa Bunge wa Novemba mwaka jana (2020), ambapo kwa mujibu wa matokeo, chama tawala cha National League for Democracy (NLD) kinachoongozwa na Aung San Suu Kyi kiliibuka na ushindi.