Apr 12, 2021 08:11 UTC
  • Baadhi ya nchi za Kiislamu kuanza mfungo wa Ramadhani kesho Jumanne

Kesho Jumanne tarehe 13 Aprili itasadifiana na siku ya kwanza ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani katika baadhi ya nchi za Kiislamu.

Nchi za Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Bahrain, Kuwait, Palestina, Misri, Oman, Jordan, Lebanon na Tunisia zimetangaza kuwa, kesho Jumanne itakuwa siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. 

Aidha nchini Indonesia, Uturuki na Mauritania kumetangazwa kuwa, kesho Jumanne itakuwa siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Wakati huo huo, baadhi ya mataifa ya Kiislamu yametangaza kuwa, Jumatano ya kesho kutwa itakuwa siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Wanazuoni na wataalamu wakiutafuta mwezi mwandamo

 

Nchini Iran Hujjatul Islam Ali Ridha Movahidnejad Mjumbe wa Kamati ya Kutafuta Mwezi ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kuna makundi takribani 100 katika maeneo mbalimbali ya nchi ambayo yanafuatilia mwandamo wa mwezi wa Ramadhani na kwamba, kuna uwezekano Jumatano ya kesho kutwa ikawa siku ya kwanza ya mwezi wa Ramadhani hapa nchini.

Radio Tehran, Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inawaombea na kuwatakia Waislamu wote duniani kheri na baraka za mwezi huo mtukufu ambao ni hiba, atia na zawadi kubwa sana inayotoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya waja wake anaowapenda.