Apr 14, 2021 02:22 UTC
  • Kukiri Biden juu ya kuudhiwa na kubughudhiwa Waislamu nchini Marekani

Rais Joe Biden wa Marekani amekiri katika ujumbe wake kwa mnasaba wa kuwadia mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani juu ya kuudhiwa na kubughudhiwa Waislamu katika jamii ya Marekani.

Biden ameandika katika ujumbe wake huo kwamba: Waislamu  wa Marekani wamekuwa wakiandamwa na vitendo vya maudhi, bughudha, taasubi na jinai zenye msukumo wa chuki; vitendo hivi  dhidi ya Waislamu ni makosa hivyo vinapaswa kukomeshwa.

Ubaguzi dhidi ya jamii za walio wachache katika jamii ya Marekani ni jambo ambalo limekuwa likiripotiwa kwa muda sasa kiasi kwamba, licha ya kuweko mchanganyiko wa jamii katika nchi hiyo na kuweko asilimia kubwa ya jamii, dini na kaumu mbalimbali, lakini jamii hizo daima zimekuwa zikikabiliwa na mbinyo na vitisho.

Waislamu ambao wanaunda asilimia moja ya jamii ya Marekani katika miaka ya hivi karibuni, wameandamwa na mateso, bughudha na ubaguzi hususan katika kipindi cha utawala wa Rais Donald Trump. Kipindi cha uongozi wa Trump kilishuhudiwa Waislamu wa Marekani wakikabiliwa na maudhi, hujuma na ubaguzi kuliko wakati wowote ule.

Maandamano dhidi ya Waislamu

 

Licha ya kuwa hali ya kujiona bora Wamarekani daima imekuweko na historia ya nchi hiyo imejaa dhulma na ukandamizaji dhidi ya watu wenye asili katika nchi hiyo lakini wasio wazungu, kama wahindi wekundu, jamii za dini za wachache na uenezaji ubaguzi, lakini baada ya mashambulio ya Septemba 11, anga ya kisiasa na kijamii ya Marekani ilibadilika na kuwa dhidi ya Waislamu siku baada ya siku. Baadhi ya viongozi wa nchi hiyo waliutaja Uislamu kuwa ni vitendo vya utumiaji mabavu au hata ni ugaidi. Hali hiyo ilizifanya fikra za waliowengi nchini Marekani kuanza kuwa dhidi ya Waislamu.

Mohsen Bazargan, mtafiti wa masuala ya jamii za walio wachache nchini Marekani anasema: Uislamu wa kuchupa mipaka ambao sisi katu hatuutambui, uliarifishwa na vyombo vya habari vya Marekani kama nembo ya Uislamu na Waislamu. Hatua hii ilipelekea magenge ya wazungu yenye chuki na taasubi na kuanza kuwaandama Waislamu na hivyo kuanzisha anga kubwa ya chuki dhidi ya Uislamu nchini Marekani.

Hali hiyo ilidhihirika zaidi baada ya kuingia madarakani Donald Trump ambapo vitendo na misimamo iliyo dhidi ya kaumu za wachache hususan Wamarekani wenye asili ya Afrika na wafuasi wa dini za walio wachache ilishadidi mno.

Maandamano ya kupinga chuiki dhidi ya Uislamu

 

Trump alitangaza rasmi misimamo iliyo dhidi ya Waislamu na akapiga marufuku kuingia nchini Marekani raia wa kigeni ambao akthari yao ni Waislamu. Katika hotuba zake mbalimbali alitangaza misimamo iliyo dhidi ya Waislamu na wahajiri walioko nchini Marekani na kuwataja kuwa wagonjwa wa kisaikolojia au magaidi.

Baada ya kusambaa virusi vya corona katika jamii ya Marekani, ubaguzi ulidhihirika hata katika sekta ya afya. Ripoti ya Kaiser Family Foundation ambayo ni moja ya asasi za kiutafiti nchini nMarekani inaonyesha kuwa, Wamarekani wenye asili ya Afrika na Wamarekani wa kaumu nyingine ambao sio wazungu wanabaguliwa mno katika suala zima la utoaji chanjo ya corona.

Waislamu wanabaguliwa na kuandamwa na vitendo vya maudhi na bughudha katika jamii ya Marekani katika hali ambayo, wengi miongoni mwao wamefanikiwa kufikia daraja za juu za kielimu, kimasomo na kijamii na kufanikiwa kutoa huduma yenye faida kwa mwanadamu na jamii ya Marekani.

Donald Trump, mwanasiasa ambaye katika kipindi cha uongozi wake kama Rais wa Marekani alitangaza wazi chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu

 

Waislamu wengi wanafanya kazi katika vituo vya elimu, vyuo vikuu na vituo vya utaifiti. Katika uga wa kisiasa pia, licha ya mashinikizo yote, lakini Waislamu wamekuwa na harakati katika uwanja huo. Rashida Tlaib na Ilhan Omar ni wawakilishi Waislamu katika Kongresi ya Marekani ambao licha ya kudhalilishwa na kuandamwa na vitisho mara chungu nzima lakini wangalipo katika medani ya kisiasa na kijamii nchini Marekani.

Licha ya kuwa, Rais Joe Biden wa Marekani katika miezi ya hivi karibuni amezungumzia suala la kupambana na ubaguzi na kufanya juhudi za kuboresha hali hiyo; lakini inaonekana kuwa, hadi sasa hakujaandaliwa mazingira mwafaka nchini Marekani kwa ajili ya jamii za walio wachache wakiwemo Waislamu.

Tags