Apr 14, 2021 02:35 UTC
  • Marekani yasimamisha chanjo ya corona ya Johnson & Johnson kwa hofu ya kuganda damu

Marekani imesitisha matumizi ya chanjo ya virusi vya corona iliyotengenezwa na kampuni ya dawa ya nchi hiyo, Johnson and Johnson, ambayo kuna madai kuwa inasababisha kuziba kwa mishipa kama matokeo ya tatizo la kuganda kwa damu kwa watu waliopewa chanjo hiyo.

Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa nchini humo (CDC) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (FDA) jana Jumanne zilisitisha matumizi ya chanjo ya Johnson & Johnson ya kuzuia Covid-19 baada ya watu sita waliopewa chanjo hiyo kupata tatizo nadra linalojumuisha kuganda kwa damu, karibu wiki mbili tuu baada ya kupewa chanjo hiyo. Hatua hiyo imechukuliwa ili kufanya uchunguzi kuhusu athari mbaya zilizojitokeza baada ya matumizi ya chanjo hiyo ya Johnson & Johnson.

Siku chache zilizopita pia Shirika la Udhibiti wa Dawa la Wakala wa Umoja wa Ulaya (EU), limeanzisha uchunguzi wa kujua endapo chanjo ya corona iliyotengenezwa na kampuni ya dawa ya Marekani ya Johnson and Johnson inasababisha kuziba kwa mishipa kama matokeo ya tatizo la kuganda kwa damu.

Kwa mujibu wa The New York Times, watu waliotumia chanjo ya Johnson and Johnson na kupatwa na tatizo la kuganda kwa damu ni wanawake sita wenye umri wa kati ya miaka 18 na 48, na kwamba mmoja wao amefariki dunia na mwingine yuko hospitalini.

Kusitishwa matumizi ya chanjo hiyo ya Kimarekani kunaweza kutoa changamoto kubwa kwa nchi za Kiafrika ambazo zinasubiri kwa hamu chanjo hiyo.

Mapema mwezi huu wa Aprili, Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika (AfricaCDC) kilitangaza makubaliano ambayo yataiwezesha kampuni ya kutengeneza na kutayarisha madawa ya Afrika Kusini, Aspen Pharmacare, kutoa hadi dozi milioni 220 kwa nchi 55 wanachama wa AU kuanzia mwezi Oktoba.

Umoja wa Afriika AU ulichukua hatua hiyo baada ya kusitisha mpango wake wa kuagiza chanjo ya AstraZeneca inayotngenezwa na Uingereza na Sweden kutokana na kugundulika kwamba, chanjo hiyo inasababisha matatizo ya kuganda kwa damu.

Katika taarifa yake ya mapema mwezi huu, Wakala wa Kudhibiti Madawa Uingereza (MHRA) ulisema watu saba kati ya 30 waliopata matatizo ya kuganda damu baada ya kupewa chanjo ya AstraZeneca, wameaga dunia.

Mwezi uliopita wa Machi, nchi kadhaa za Ulaya pia zilisimamisha matumizi ya chanjo ya kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19 ya AstraZeneca kutokana na madhara yake kwa damu za watu waliopewa chanjo hiyo.

Tags