Apr 15, 2021 08:15 UTC
  • Mauzo ya silaha ya serikali ya Biden kwa Imarati

Miezi kadhaa ikiwa imepita tokea Joe Biden atangaze kusimamisha na kutazmwa upya mkataba wa mauzo ya silaha za Marekani kwa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), rais huyo mpya wa Marekani ametangaza kuwa ataendelea na mpango wa awali wa kuiuzia nchi hiyo ya Kiarabu silaha zenye thamani ya dola bilioni 23, ikiwa ni pamoja na ndege za kivita aina ya F35, droni zenye kubeba silaha na zana nyinginezo za kivita

Donald Trump, rais wa zamani wa Marekani alikubali kuiuzia Imarati silaha hizo mara tu baada ya nchi hiyo ya Kiarabu kutangaza kuutambua rasmi utawala ghasibu wa Israel. Mkataba huo ulitiwa saini katika hali ambayo Imarati na Saudi Arabia zilikosolewa vikali na mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu na raia wa nchi nyingine kutokana na hatua yao ya kuendelea kuwaua kwa umati watu wa Yemen, tena katika mazingira magumu ya kuenea duniani janga la virusi vya corona. Mashirika hayo huku yakifichua maafa na jinai kubwa inayotekelezwa na nchi mbili hizo za Kiarabu na washirika wao wa Magharibi dhidi ya raia masikini wa Yemen, ambao hawana mtu wa kuwatetea, yalizitaka nchi zinazoziuzia silaha Saudia na Imarati na hasa Marekani na nchi za Ulaya, zisimamishe mara moja mauzo hayo ya silaha zinazotumika kuwaua kikatili Wayemen. Licha ya maombi na matakwa hayo ya jamii ya kimataifa lakini utiwaji saini mkataba huo wa mauzo ya silaha ulikuwa ushindi mkubwa kwa Imarati na Saudia kwa ajili ya kuzipatia silaha mpya na za kisasa katika jinai yao ya kuendelea kuwaua Kinyama raia wa Yemen wasio na hatia, na hasa watoto na wanawake.

Imarati, Marekani na Israel zikitia saini mapatano ya UAE kuutambua rasmi utawala haramu wa Israel

Pamoja na kuwa mauzo ya silaha hizo yalipingwa na wajumbe wa mabunge yote mawili ya Congerss na Seneti ya Marekani lakini Trump kutokana na kiburi chake alitumia uwezo wake wa veto dhidi ya pinzani huo na kuamua kusukuma mbele mauzo ya silaha hizo kwa hoja kuwa kama hangelifanya hivyo uhusiano wa Marekani na nchi mbili hizo za Kiarabu ungetumbukia hatarini. Hii ni katika hali ambayo isipokuwa nchi wanachama wa Nato, Japan na Korea Kusini, katika eneo zima la Asia Magharibi, ni utawala ghasibu wa Israel tu ndio hadi sasa umekuwa na fursa ya kutumia ndege hizo za F35.

Akiwa katika kampeni za uchaguzi wa Marekani, Biden aliahidi kwamba kama angechaguliwa kuwa rais wa Marekani, angechunguza upya na hatimaye kufutilia mbali mkataba wa mauzo ya silaha kwa Imarati, jambo ambalo liliwavutia wengi. Hata baada ya kuchaguliwa kuwa rais wa Marekani, Biden alisema alikuwa amesimamisha kwa muda mkataba huo kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi. Watu wengi duniani, na hasa mashirika ya kutetea haki za binadamu, waliupokea vizuri uamuzi wake huo ambapo hata viongozi mashuhuri nchini Marekani walimpongeza kwa uamuzi wake huo ulioonekana kuwa wa busara.

Seneta Elizabeth Warren, akibainisha furaha yake kutokana na uamuzi wa Biden wa kusimamisha kwa muda mauzo ya silaha kwa Imarati na Saudi Arabia ili kufanyika uchunguzi zaidi alisema: Nchi mbili hizo ndio wahusika wakuu wa maafa ya kibinadamu yanayoendelea Yemen, kwa kuendelea kufanya kwa miaka mingi, mashambulio ya mabomu yasiyo na maana dhidi ya nchi hiyo.

Licha ya makaribisho na maombi hayo yote, lakini sasa imebainika wazi kwamba ahadi hizo za Biden hazikuwa lolote ila nara tupu zisizokuwa na maana yoyote. Ni wazi kuwa nara hizo zilikuwa propaganda za kisiasa tu zilizokusudiwa kuhadaa fikra za waliowengi na hatimaye kupata uungaji mkono wa mashirika ya kutetea haki za binadamu katika juhudi zake za kutafuta urais wa Marekani.

Seneta Elizabeth Warren

Philippe Nassif, mkuu wa kanda ya Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika katika Shirika la Msamaha Duniani, Amnesty International, anasema kuhusu suala hilo kuwa: Miaka sita imepita tokea vita vya Yemen vianze na daima nimekuwa nikikosoa na kulalamikia namna silaha zinavyovushwa na kupelekwa Yemen kwa njia isiyo ya uwajibikaji. Tunazionya nchi za Magharibi kuhusu chokochoko zao huko Yemen kwamba kuendelea kuupa silaha muungano wa Kiarabu unaoongozwa na Saudia ni kushiriki katika jinai za kivita nchini humo.

Pamoja na nara zote zilizotolewa katika uwanja huo, lakini uamuazi wa karibuni wa Biden wa kuiuzia silaha Imarati unathibitisha wazi kwamba kuna magenge makubwa ya kimafia na lobi za silaha zenye ushawishi mkubwa nchini Marekani ambazo hazijali hata kidogo thamani za kiutu na haki za binadamu bali hufikiria tu jinsi zitakavyotengeneza pesa na kupata faida nono katika uwanja huo. Hii ni pamoja na kuwa licha ya madbadiliko ya uongozi na kisiasa yaliyotokea Marekani lakini bado nchi hiyo ni muungaji mkono mkubwa wa Saudi Arabia na Imarati katika vita, jinai na mauaji ya kinyama zinayoyatekeleza dhidi ya watu wa Yemen.

 

Tags