Apr 15, 2021 12:45 UTC
  • Mkuu wa CIA: Marekani inajitia hatarini kuwaondoa askari nchini Afghanistan

Mkuu wa shirika la ujasusi la Marekani CIA amesema, nchi hiyo inajihatarisha kwa kuchukua uamuzi wa kuwaondoa askari wake nchini Afghanistan.

William J. Burns ameyasema hayo katika taarifa, akiashiria uamuzi uliotangazwa na Rais wa Marekani Joe Biden wa kuwaondoa askari wa jeshi la nchi hiyo walioko nchini Afghanistan na kusisitiza kuwa, kwa kuondoka askari wa Marekani nchini humo, uwezo wa Washington wa kukabiliana na vitisho utapungua kwa kiwango fulani.

Mkuu wa shirika la ujasusi la Marekani ameongeza kuwa, "kuondoka vikosi vya jeshi la Marekani nchini Afghanistan maana yake ni sisi kukabiliwa na hatari."

Williams Burns

Rais Joe Biden wa Marekani alitangaza Jumatano kwamba, askari wa jeshi la nchi hiyo wataondolewa nchini Afghanistan na akaeleza kuwa, wakati umewadia wa kuhitimisha vita virefu zaidi ambavyo Marekani ilikuwa imejitumbukiza ndani yake.

Kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi, Marekani iliishambulia na kuivamia kijeshi Afghanistan mwaka 2001 na kuuangusha utawala wa wakati huo wa kundi la Taliban. Hata hivyo, baada ya kupita miaka 20 na kupata nguvu tena kundi la Taliban; na kufuatia makubaliano ya amani ambayo serikali iliyopita ya Marekani ya Donald Trump ilisaini na kundi hilo mjini Doha, Qatar, hivi sasa Biden amekuwa hana njia nyingine isipokuwa kuhitimisha vita hivyo, bila Marekani kupata mafanikio yoyote kwa kuivamia kijeshi Afghanistan, ikiwa pia imeshindwa vibaya zaidi nchini humo kuliko ilivyoshindwa katika vita na uvamizi wa Vietnam.

Vita vya Afghanistan vimeigharimu Washington dola trilioni mbili na bilioni 400.../

Tags