Apr 16, 2021 07:52 UTC
  • Araqchi: Nchi za Ulaya zinapaswa kuonyesha zinayapa uzito mazungumzo ya nyuklia

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Tume ya Pamoja ya Mapatano ya Nyuklia ya JCPOA ilifanya kikao chake Vienna, Austria jana Alhamisi ambapo kikao hicho kilikuwa na changamoto nyingi.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa, nchi za Ulaya zinapaswa kuonyesha kuwa zinayapa uzito mazungumzo hayo ya nyuklia. Araqchi amesema Iran haina hamu ya kushiriki katika mazungumzo yatakayodumu kwa muda mrefu na kuongeza kuwa, tunapaswa kuona hatua za kivitendo zinazoashiria kufikiwa mapatano na kasi ya mazungumzo iwe ni yenye kukubalika kinyume na hivyo Iran haioni haja ya kuendelea na mazungumzo.

Araqchi pia ameashiria tukio la kigaidi katika kituo cha nyuklia cha Natanz na kusema: "Hatuwezi kuacha tukio hilo lipite kirahisi."

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayeshughulikia masuala ya kisiasa ameendelea kusema kuwa, Iran inataraji tukio hilo la Natanz litalaaniwa na nchi za Magharibi. Amesema mbali na Russia na China, nchi tatu za Ulaya zinazoshiriki katika mazungumzo na Iran yaani, Uingereza, Ujerumani na Ufaransa, si tu kuwa hazikulaani tukio hilo bali zimeongeza vikwazo dhidi ya Iran. Araqchi amesema vikwazo hivyo vimepelekea Iran itilie shaka nia ya nchi za Ulaya.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema iwapo nchi za Ulaya na Marekani hazitatekeleza ahadi zao, Iran nayo pia haitatekeleza ahadi zake.

Duru mpya ya mazungumzo ya nyuklia baina ya Iran na kundi la 4+1 ilianza siku kumi zilizopita huko Vienna kwa shabaha ya kuhuisha makubaliano ya JCPOA na kufutwa vikwazo vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, baada ya Tehran kujihakikishia kwamba, vikwazo hivyo vimefutwa kivitendo.

Iran inasisitiza kuwa, kuondolewa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ambavyo viliwekwa wakati wa utawala wa rais wa zamani wa nchi hiyo, Donald Trump, ni hatua ya dharura kwa ajili ya kuhuisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA;

Tags