Apr 16, 2021 08:00 UTC
  • WHO: COVID-19 imeua watu zaidi ya milioni moja Ulaya, hali bado ni mbaya

Shirika la Afya Duniani, WHO limetangaza kuwa watu waliopoteza maisha kutokana na COVID-19 au corona barani Ulaya wamepindukia milioni moja.

Mkurugenzi wa WHO barani Ulaya, Daktari Hans Kluge amesema hali bado ni mbaya, na ametaka wakazi wa bara hilo waendelee kuzingatia kanuni za kuzua kuenea COVID-19. Aidha amezitaka nchi kuharakisha mchakato wa chanjo huku aina mpya za kirusi cha COVID-19 zikipelekea maambukizi kuongezeka.

Daktari Hans Kluge amesema takriban visa vipya milioni 1.6 vya virusi vya corona vikirekodiwa katika bara hilo kila wiki.

Nayo ripoti mpya ya Chuo Kikuu cha John Hopkins inaonyesha kuwa karibu watu milioni tatu wamepoteza maisha kutokana na corona duniani ambapo Marekani ndio imeathiriwa vibaya zaidi ikifuatiwa na bara Ulaya.

Kampeni ya kukomesha corona nchini Kenya

Kwingineko, Kituo cha Kukinga na Kudhibiti Maradhi cha Afrika (Africa CDC) kimesema nchi za Afrika zimefanya vipimo milioni 41 vya COVID-19 hadi sasa. Aidha ripoti ya Africa CDC inaonyesha  ongezeko la asilimia 2.4 la vipimo wiki iliyopita ikilinganishwa na wiki iliyotangulia, huku kiwango cha watu wanaogunduliwa kuwa na matokeo chanya au waliopatikana na COVID-19 kikiwa kimefikia asilimia 10.2.

Kituo hicho kimesema katika ripoti mpya kuwa watu milioni 4.3 wamegunduliwa kuambukizwa COVID-19, na hadi sasa idadi ya watu waliokufa kwa ugonjwa huo imefikia laki 1.16, na wengine waliopona imefikia milioni 3.9.

Afrika Kusini, Morocco, Tunisia, Ethiopia na Misri ndio nchi zilizoathiriwa zaidi na ugonjwa huo, na kwa upande wa maeneo, eneo la Kusini mwa Afrika ndio limeathiriwa zaidi, likifuatiwa na eneo la Mashariki, huku eneo la kati likiwa limeathiriwa kidogo zaidi.

 

Tags