Apr 16, 2021 12:05 UTC
  • Maria Zakharova
    Maria Zakharova

Russia imeikosoa vikali serikali ya Marekani ikisema kuwa itajibu mapigo kwa vikwazo vipya vya nchi hiyo vilivyotangazwa na Rais Joe Biden dhidi ya Moscow.

Msemaji wa Wizara  Mambo ya Nchi za Nje ya Russia, Maria Zakharova amesema, Marekani inapaswa kutambua kuwa, italipa gharama kubwa kutokana na kuendelea kuharibu uhusiano wa pande hizo mbili. 

Zakharova amesema kuwa, Washington haiko tayari kukubali uhakika kwamba, kuna ulimwengu wenye kambi kadhaa usiokubali udhibiti na ukiritimba wa Marekani. Amesisitiza kuwa, Russia itaoa jibu kwa siasa hizo za Marekani.

Marekani imewafukuza wanadiplomasia 10 wa Russia waliokuwa wakifanya kazi mjini Washington na ikayawekea vikwazo mashirika na shakhsia kadhaa wa Russia wanaotuhumiwa kuwa waliingilia uchaguzi wa rais wa Marekani mwaka 2016. 

Russia inapinga ukiritimba wa Marekani

Wakati huo huo Ikulu ya Rais wa Russia, Kremlin, imetangaza kuwa, vikwazo hivyo vipya vya Marekani vinapunguza uwezekano wa kufanyika mkutano baina ya marais Joe Biden na Vladimir Putin. Pendekezo la kufanyika mkutano huo limetolewa na Rais wa Marekani kwa ajili eti kuboresha uhusiano unaozidi kuharibika wa nchi hizo mbili.

Russia imekanusha madai ya kuingilia uchaguzi wa rais wa Marekani mwaka 2016 au kuhusika na hujuma yoyote ya kimtandao dhidi ya nchi hiyo.      

Tags