Apr 17, 2021 02:41 UTC
  • Hati ya ushirikiano mpana wa kistratijia wa Iran na China na wasiwasi wa Wamagharibi

Tarehe 29 Machi mwaka huu, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na China walitia saini hati ya ushirikiano mpana wa kistratijia wa nchi mbili, kufuatia safari ya Wang Yi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China mjini Tehran, ikiwa ni katika kukaribia maadhimisho ya kutimia miaka 50 ya uhusiano wa kidiplomasia wa Tehran na Beijing.

Licha ya kuwa ni muda sasa tokea kutiwa saini hati hiyo lakini bado vyombo vya habari vya Magharibi vinachambua na kutathmini suala hilo kwa kina. La muhimu hapa ni kwamba vyombo vya habari vya nchi za Magharibi vimelipa uzito mkubwa suala hilo na kuamua kuangazia ushirikiano wa Iran na China kwa mtazamo hasi na wa kipropaganda.

Swali linalojitokeza hapa ni kwamba je, ni kwa nini nchi na viongozi wa Magharibi wamekerwa, kuchukizwa na hata kuwa na hofu kubwa kuhusiana na ushirikiano wa nchi mbili hizi? Kuna nukta kadhaa zinazopaswa kuzingatiwa katika uwanja huo.

Nukta ya kwanza ni kuwa wachambuzi na wajuzi wengi wa masuala ya kisiasa na kiuchumi wanakubaliana kwamba kutiwa saini hati hiyo ya ushirikiano wa Iran na China ni moja ya matukio muhimu zaidi katika uwanja wa siasa za nje za Iran katika mwaka huu wa Kiirani wa 1400 Hijiria Shamsia. Pamoja na kuwa hati hiyo ilitiwa saini tarehe 26 Machi lakini ni wazi kuwa hujudi za kufikiwa hatua hiyo zimefanywa na viongozi wa nchi mbili kwa zaidi ya miaka mitano iliyopita.

Nukta ya pili ni kuwa kama inavyoashiria anwani ya hati yenyewe iliyofanyiwa kazi kwa muda mrefu, pande mbili zimeamua kunyanyua uhusiano na ushirikiano wao katika nyanya zote ili kufikia hatua ya mashirikiano ya kistratijia kiutendaji.

Baada ya kutiwa saini hati ya ushirikiano wa kistratijia kati ya Iran na China

Kwa hakika hati hiyo inapasa kuchukuliwa kuwa ni mpango wa kisiasa, kiuchumi, kistratijia, na kiutamaduni katika nyanja zote kwa ajili ya kuimarisha uhusiano wa muda mrefu. Kutiwa saini hati hiyo ya ushirikiano wa kistratijia katika mkesha wa maadhimisho ya miaka 50 ya uhusiano wa kidiploamsia wa pande mbili ni hatua ya kihistoria katika uhusiano wa nchi mbili.

Kwa mtazamo wa vyombo vya habari vya Magharibi, moja ya sababu za Marekani kupinga uimarishwaji ushirikiano wa Iran na China ni kuwa jambo hilo litapelekea kudhoofishwa mashinikizo ya kiwango cha juu ya nchi hiyo dhidi ya Iran. Kuhusu suala hilo, gazeti la Marekani la Wall Street Journal limeandika kwamba hati hiyo ya ushirikiano inalenga kupunguza mashinikizo ya Marekani dhidi ya nchi mbili hizi ambazo zimethibitisha kivitendo kwamba zina njia mbadala ya kukabiliana na mashinikizo hayo.

Gazeti jingine la Marekani la New York Times nalo linasema kwamba iwapo hati hiyo itakamilika na kutekelezwa kivitendo, itatoa pigo kubwa kwa juhudi za mashinikizo ya juu na siasa za vitisho za Marekani dhidi ya Iran.

Gazeti la al-Misr al-Yaum nalo linasema kwamba utiwaji saini hati ya ushirikiano kati ya Iran na China utafanya vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran vishindwe kufikia malengo yanayokusudiwa, na kuongeza kuwa rais wa Marekani ana haki ya kutangaza wasiwasi alionao kuhusu hati hiyo kwa sababu inanyanyua ushirikiano wa nchi mbili kufikia kiwango cha muungano wa nchi mbili ambao bila shaka utadhoofisha pakubwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran.

Wakati huo huo, Abdulbari Atwan mchambuzi na mwandishi mashuhuri wa ulimwengu wa Kiarabu anasema kuhusu hati ya ushirikiano wa kistartijia kati ya Iran na China kwamba, mkataba mpya kati ya nchi mbili hizi umemuweka Rais Biden wa Marekani katika hali ngumu na kumfanya ajihisi kuwa dhaifu. Kuhusu suala hilo kanali ya ABC ya Marekani inasema kwamba huo ni mktaba wa kwanza wa ushirikiano wa kistratijia wa muda mrefu kuwahi kuwekwa kati ya Iran na moja ya nchi zenye nguvu kubwa duaniani. Shirika la habari la Bloomberg linasema hiyo ni changamoto kubwa kwa Rais Biden ambaye anajaribu kuunda muungano wa kimataifa kwa ajili ya kukabiliana na China.

Mbali na sababu hizo zinazotolewa na vyombo vya habari vya Magharibi kuna sababu nyingine ambazo zinatolewa na vyombo vya habari vya utawala haramu wa Israel kuhusu hati hiyo. Gazeti la utawala huo la Jerusalem Post limeandika kwamba kutiwa saini hati ya ushirikiano wa kistratijia kati ya Iran na China ni habari mbaya mno kwa Isreal, habari ambayo huenda ikawa mbaya zaidi katika siku zijazo.

Safari iliyofanywa mjini Tehran miaka mitano iliyopita na Rais Xi Jinping wa China kujadili hati hiyo

Gazeti la Haaretz nalo limechambua kwa kina hati hiyo na kusema inaweka wazi kushindwa siasa za Donald Trump rais wa zamani wa Marekani na Benjamini Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel dhidi ya Tehran. Gazeti hilo la Kizayuni linasema kuwa mapatano ya ushirikiano wa muda mrefu kati ya China na Iran yanathibitisha kwamba licha ya mashinikizo na vikwazo vikali vya Marekani dhidi ya Iran lakini serikali ya Tehran ingali ina muda mrefu kabla ya kupigishwa magoti na nchi za Magharibi.

Gazeti la Global Times pia limetoa ripoti kuhusu utiwaji saini hati hiyo na kusema kwamba ukandamizaji na siasa za mabavu za Marekani hazijazuia ushirikiano wa China na Iran pamoja na nchi nyingine za Mashariki ya Kati. Linasema, siasa hizo badala ya kufikia malengo yaliyokusudiwa zimepelekea tu nchi za eneo kuanzisha na kuimarisha ushirikiano wao kwa maslahi ya kitaifa.

Hakika licha ya uchochezi na propaganda zinazoenezwa na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi kuhusu hati ya ushirikiano wa kistratijia kati ya China na Iran, lakini vyombo hivyo hivyo vimeashiria kwa njia isiyo ya moja kwa moja faida zinazopatikana katika hati hiyo kwa maslahi ya nchi za eneo yakiwemo ya kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni, kiusalama na kiulinzi.

Wajuzi wa mambo wanasema kuwa juhudi kubwa ambazo zimefanywa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika miaka ya karibuni zikiwemo za kuleta usalama na uthabiti wa kisiasa katika nchi za Syria na Iraq, kutokomeza kundi la kigaidi la Daesh katika nchi hizo, kuwaunga mkono kimaanawi watu wa Yemen katika mapambano yao ya miaka sita dhidi ya uvamizi wa muungano wa kijeshi wa Saudia, uwezo mkubwa wa kijeshi wa Iran na kusimama kwake imara mbele ya vikwazo na mashinikizo ya kiwango cha juu ya Marekani ni baadhi ya mambo ambayo yameifanya China iwe na hamu ya kuanzisha uhusiano na ushirikiano wa kistratijia wa muda mrefu na serikali ya Tehran, katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kiusalama.

 

 

Tags