Apr 17, 2021 03:29 UTC
  • Russia yawafukuza wanadiplomasia 10 wa Marekani kujibu vikwazo vya Washington

Katika kujibu mapigo kwa hatua ya uhasama na vikwazo vipya vya Washington vilivyotangazwa hivi karibuni na Rais Joe Biden dhidi ya Russia, serikali Moscow imewatimua nchini humo wanadiplomasia kumi wa Marekani.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje ya Russia, Sergey Lavrov amesema mbali na Moscow kuwafukuza wanadiplomasia kumi wa Marekani nchini humo, lakini pia imewaweka maafisa wanane wa Washington katika orodha yake ya vikwazo.

Lavrov amesema shakhsia na maafisa wa ngazi za juu waliowekewa vikwazo na Moscow ni pamoja na walioko katika utawala wa sasa na uliopita wa Marekani, kwa ama kushinikiza au kutekeleza sera za uhasama za US dhidi ya Russia.

Amesema tayari Russia imemuagiza John Sullivan, Balozi wa Marekani mjini Moscow aondoke nchini humo na arejee Washington kwa ajili ya kile kilichotajwa kuwa mashauriano. Lavrov amesema hatua hizo zilizochukuliwa na Russia ni jibu kwa hatua za uhasama za utawala Washington dhidi ya Moscow.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje ya Russia, Sergey Lavrov

Haya yanajiri siku chache baada ya Marekani kuwafukuza wanadiplomasia kumi wa Russia waliokuwa wakifanya kazi mjini Washington na ikayawekea vikwazo mashirika na shakhsia kadhaa wa Russia wanaotuhumiwa kuwa waliingilia uchaguzi wa rais wa Marekani wa mwaka 2016. Russia imekanusha madai ya kuingilia uchaguzi huo wa rais wa Marekani au kuhusika na hujuma yoyote ya kimtandao dhidi ya nchi hiyo. 

Ikulu ya Rais wa Russia (Kremlin) imetangaza kuwa, vikwazo hivyo vipya vya Marekani vinapunguza uwezekano wa kufanyika mkutano baina ya marais Joe Biden na Vladimir Putin. Pendekezo la kufanyika mkutano huo limetolewa na Rais wa Marekani kwa ajili eti kuboresha uhusiano unaozidi kuharibika wa nchi hizo mbili.

 

Tags