Apr 21, 2021 07:29 UTC
  • Mbunge wa Bunge la Ulaya: Tofauti na US, Iran iliisaidia Iraq kupambana na ISIS

Mbunge wa kujitegemea wa Bunge la Ulaya (MEP) amesema kuibuka kundi la kigaidi la ISIS (Daesh) nchini Iraq ni matokeo ya Marekani kuivamia nchi hiyo ya Kiarabu mwaka 2003; na kwamba kinyume na Marekani, Iran iliinyooshea Baghdad mkono wa msaada na uungaji mkono katika vita dhidi ya genge hilo la kitakfiri.

Mick Wallace ambaye ni raia wa Ireland alisema hayo jana katika ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kubainisha kuwa, Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama alikataa kuipa Iraq msaada, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilimsaidia jirani yake huyo katika makabiliano na ISIS.

Wallace ameandika: Daesh ilishamiri kwa kuharibiwa Iraq, kutokana na uvamizi ulio kinyume cha sheria wa Marekani, ambapo wanachama wengi walitokea katika magereza walikokuwa wakiteswa na Wamarekani. 

Mwanasiasa huyo wa Ulaya ameongeza kuwa, "wakati ambapo Iraq ilimuomba Obama msaada wa kukabiliana na ISIS, alikataa, lakini Iran ilikubali."

Trump amewahi kukiri mara kadhaa kuhusu nafasi ya US ya kuundwa ISIS

Mbunge huyo wa kujitegemea wa Bunge la Ulaya amebainisha kuwa, Marekani, utawala (haramu) wa Israel pamoja na waitifaki wao katika eneo la Ghuba ya Uajemi waliyapa silaha magenge ya kitakfiri ili yaibue hali ya mchafukoge nchini Syria.

Huko nyuma pia, mbali na kukosoa nafasi haribifu ya Umoja wa Ulaya katika kuvamiwa Iraq, Wallace amewahi kupongeza hatua ya Iran ya kuviunga mkono vikosi vya kujitolea wananchi (Hashdu Shaabi) katika kupambana na ISIS nchini Iraq. 

 

Tags