Apr 23, 2021 05:59 UTC
  • Guterres alalamikia ubaguzi wanaofanyiwa watoto wa kike na wanawake katika teknolojia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelalamikia vikali ubaguzi wanaofanyiwa watoto wa kike na wanawake katika Teknolojia za Habari na Mawasiliano kwa kifupi TEHAMA licha ya kwanza teknolojia hiyo ni muhimu sana wakati huu wa janga a Corona, au COVID-19.

António Guterres amesema, licha ya teknolojia hiyo kuwa na umuhimu mkubwa katika kuunganisha watu na vile vile kusongeza karibu biashara na huduma muhimu, lakini bado nusu ya wakazi wa dunia hawajauniganishwa kwenye mtandao na wengi wao wanaokosa huduma hiyo ni wanawake na wasichana kwenye nchi zinazoendelea.  

Amesema, takwimu za hivi karibuni kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la mawasiliano duniani, ITU zinaonesha kuweko pengo la asilimia 17 la matumizi ya Intaneti kote ulimwenguni. Pengo hilo ni kubwa zaidi katika nchi maskini. Katika maeneo mengine, pengo la ukosefu wa mtandao kijinsia ni kubwa zaidi na hivyo kuongeza ukosefu wa usawa na kuwanyima wanawake na wasichana fursa za kupata elimu, ajira bora na hata kushindwa kufanya biashara. 

 

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameyataka mataifa ya dunia kutia nia ya kweli ya kutatua tatizo hilo. Amesema: “Hebu leo tuazimie tena kwenye lengo la kuwa na fursa sawa kwa vijana wa kike na watoto wa kike katika sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati, STEM.” 

Vile vile amesema, suala la kila mtu kuweza kupata teknolojia hizo ni jambo muhimu katika kujenga jamii na uchumi na kushughulikia changamoto nyingi zinazokabili dunia hivi sasa.