Apr 23, 2021 07:34 UTC
  • Mgogoro wa kijeshi baina ya US na Russia, Marekani yapasisha msaada wa mamia ya mamilioni kwa Ukraine

Kamati ya Masuala ya Kimataifa ya Baraza la Sanate la Marekani imepasisha muswada wa kuisaidia kijeshi Ukraine kwa mamia ya mamilioni ya dola kama njia ya kukabiliana na nguvu za kijeshi za Russia katika eneo la mashariki mwa Ulaya.

Markarova Oksana, balozi wa Ukraine nchini Marekani ameandika katika ukurasa wa kijamii wa Facebook kwamba, Kamati ya Masuala ya Kimataifa ya Baraza la Sanate la Marekani imepasisha kwa kauli moja muswada wa kushirikiana na Ukraine katika masuala ya ulinzi na usalama.

Muswada huo unasema, misaada ya kijeshi ya Marekani kwa Ukraine itaongezeka hadi milioni 300 mwaka huu katika kukabiliana na nguvu za kijeshi za Russia kwenye mipaka ya Ukraine. Muswada huo ulikuwa unasubiri kupasishwa na Baraza hilo la Sanate la Marekani na sasa unasubiri saini ya rais wa nchi hiyo kupasishwa rasmi. Mivutano baina ya Marekani na Russia imeongezeka sana hivi sasa.

Mgogoro wa Russia kwa upande mmoja na Ukraine na Marekani kwa upande wa pili

 

Siku chache zilizopita, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitangaza kwamba imemtaka balozi wake aliyeko mjini Moscow Russia arejee nyumbani kwa mashauriano zaidi na viongozi wa Washington.

Wizara hiyo ilisema kwamba Balozi John Sullivan ametakiwa arudi mjini Washington wiki hii kwa ajili ya kufanya mashauriano na viongozi wa serikali mpya ya Rais Joe Biden ambao inadaiwa hajapata nafasi muafaka ya kuonana nao tokea alipochaguliwa katika nafasi hiyo ya kuhudumia serikali ya Marekani mjini Moscow, na vile vile kuonana na familia yake.

Pamoja na hayo lakini wajuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa kuna sababu nyingine nyingi na muhimu zaidi ambazo zimempelekea Balozi John Sullivan aitwe nyumbani mjini Washington. Serikali ya Marekani Alkhamisi iliyopita iliwawekea vikwazo vipya raia na mashirika 32 ya Russia.