Apr 23, 2021 11:59 UTC
  • WHO yazindua mpango wa kutokomeza ugonjwa wa malaria ifikapo 2025

Shirika la Afya Duniani (WHO) limezindua mpango kabambe wenye lengo la kutokomeza ugonjwa wa malaria katika nchi 25 duniani ifikapo mwaka 2025.

Katika kuelekea Siku ya Malaria Duniani, inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 25 Aprili,  Shirika la Afya Duniani limepongeza idadi kubwa ya nchi zinazokaribia na kufikia, utokomezaji kabisa wa ugonjwa wa malaria.

Mpango mpya uliozinduliwana shirika hilo unalenga kusitisha maambukizi ya ugonjwa huo katika nchi 25 zaidi ifikapo mwaka 2025.

Ripoti iliyotolewa na WHO inabainisha kuwa, kati ya nchi 87 zilizo na malaria, 46 ziliripoti chini ya visa 10,000 vya ugonjwa huo mwaka 2019 ikilinganishwa na nchi 26 mwaka 2000.

Aidha ripoti hiyo inaeleza kuwa, kufikia mwisho mwa mwaka jana (2020), nchi 24 ziliripoti kufanikiwa kudhibiti usambaaji wa malaria kwa miaka 3 mtawalia au zaidi na kati ya nchi hizo, 11 zilithibitishwa na WHO kutokomeza kabisa ugonjwa wa malaria.

Tarehe 25 Aprili ni Siku ya Malaria Duniani

 

Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ameziambia duru za habari kwamba:  "Nchi nyingi tunazozitambua leo, huko nyuma zilibeba  mzigo mzito  sana wa malaria. Mafanikio yao yalipatikana kwa juhudi kubwa na za miongo mingi ya hatua kadhaa. Kwa pamoja, wameuonyesha ulimwengu kwamba, kutokomeza malaria ni jambolinalowezekana kwa nchi zote."

Kwa mujibu wa WHO nchi nyingi ambazo zinafikia kiwango cha kutokomeza kabisa malaria zina mifumo madhubuti ya huduma ya afya ambayo inahakikisha upatikanaji wa kinga ya malaria, utambuzi na huduma za matibabu, bila kukabiliwa na shida za kifedha, kwa kila mtu anayeishi ndani ya mipaka ya nchi hiyo bila kujali utaifa au hadhi ya kisheria.