Apr 24, 2021 03:21 UTC
  • Onyo lisilo na kifani la Putin kwa Wamagharibi kuhusu kuvuka mistari myekundu ya Russia

Rais Vladimir Putin wa Russia amehutubu mbele ya wajumbe wa mabunge mawili ya nchi hiyo, Duma na Seneti, na magavana wa maeneo yote ya nchi hiyo ambapo ametoa onyo kali kwa nchi za Magharibi.

Amesema jibu la Russia kwa uchokozi wowote litakuwa la kasi kubwa na kali sana  na hivyo ameelezea matumaini yake kuwa hakuna nchi itakayothubutu kuvuka mistari myekundu ya Russia.

Putin ametoa kauli hiyo huku kukishuhudiwa kuanza duru mpya ya taharuki baina ya Russia na nchi za  Magharibi ambapo Marekani imeiwekea Russia vikwazo vipya.  Huku akiashiria vikwazo hivyo na hatua mpya zilizochukuliwa na Wamagharibu dhidi ya Russia kuhusu Ukraine, Putin amesema: “Waungaji mkono wa chokochoko zozoteo ambazo zinahatarisha misingi ya usalama wa taifa la Russia watakabiliwa na jibu kali sana ambalo litawafanya wajute.” Putin amezifafanisha nchi zinazokabiliana na Russia kuwa  sawa na fisi wanaoongozwa na Chui milia na kuonya kuwa Russia italinda maslahi yake katika fremu ya sheria za kimataifa.

Onyo kali na la  wazi la  Rais wa Russia kwa nchi za Magharibi hasa Marekani na waitifaki wake wa Ulaya katika muungano wa kijeshi wa NATO linatokana na matukio ya hivi karibuni baina ya Russia na madola ya Magharibi. Msuguano huo umeibuka kutokana na mgogoro wa mashariki mwa Ukraine na pia hatua ya Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya kuiwekea Russia vikwazo na kuingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo.

Murtadha Khansari, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema stratijia ya Marekani na waitifaki wake Ulaya ni kuifanya Russia itumbukie katika mgogoro na daima iwe katika hali  ya kujitetea huku ikiwa imesakamwa kwa vikwazo ili iafiki mitazamo ya Magharibi kuhusu mabadiliko ya kijiopolitiki katika eneo la Eurasia na Ulaya Mashariki.

Wamagharibi wanaituhumu Russia kuwa inawaunga mkono wale wanaotaka kujitenga katika eneo la Ukraine Mashariki na pia  wanasema kuwa Russia imetuma makumi ya maelfu ya wanajeshi na zana za kivita katika eneo la mpaka wake na Ukraine hasa eneo la Crimea.

Ukraine imewataka waitifaki wake Wamagharibi waionye Russia kuwa hatua zake hizo zitakuwa na athari mbaya.

Kwa kuzingatia hilo, Marekani na waitifaki wake wamechukua hatua za kichochezi kwa kisingizio cha ‘kuunga mkono Ukraine’ ambapo mbali na kuitumia nchi hiyo misaada ya kijeshi wametangaza kuwa tayari kutuma wanajeshi wa madola ya Magharibi nchini Ukraine. Kuhusiana na hilo, mwanachama mwandamizi wa NATO, Uingereza, imetuma meli zake za kivita katika Bahari ya Baltic kwa lengo la kuiunga mkono Ukraine.

Katika uga wa kisiasa na kidiplomasia pia, nchi za Magharibi zimeshadidisha mashinikizo dhidi ya Russia. Kwa mfano, kwa kisingizio kuwa Russia iliingilia uchaguzi wa Marekani na kutekeleza hujuma ya kimtandao, Marekani imetangaza vikwazo vipya dhidi ya watu na taasisi 32 za Russia na kutangaza kuwatimua wanadiplomasia 10 Warussia kwa tuhuma za ujasusi.

Katika kujibu uhasama huo, Russia nayo pia imetangaza kuwatimua wanadiplomasia 10 wa Marekani na pia imeweka maafisa 8 wa Marekani katika orodha yake ya vikwazo. Mgogoro katika uhusiano wa Russia na Marekani umepelekea mabalozi wa nchi hizi mbili waitwe nyumbani.

Aidha baadhi ya nchi za Ulaya kama vile Jamhuri ya  Czech  zimechukua hatua sawa na ya Marekani na kuwatimua wanadilomasia wa Russia. Katika kujibu uhasama huo Russia nayo imewatimua wanadiplomasia wa Waczech.

Rais wa Belarus Alexander Lukashenko

Wakati huo huo  nchi za Magharibi zinaingilia mambo ya ndani ya Russia kwa kisingizio cha hali mbaya ya kiafya ya Alexei Navalny kinara wa wapinzani wa serikali ya Russia. Wamagharibi wanataka kinara huyo aachiliwe huru. Huku hayo yakijiri Putin amezituhumu nchi za Maghribi kuwa zimekuwa zikitekeleza njama ya kumuua Rais wa Belarus Alexander Lukashenko ambaye ni muitifaki mkubwa wa Russia. Kitendo kama hicho pia kinahesabiwa kuwa mstari mwekundu kwa Russia.

Matukio hayo yote yamepelekea kuwepo taharuki kubwa katika uhusiano wa Russia na madola ya Magharibi. Taharuki hiyo imefika kiwango hatari sana na ambacho hakijawahi kushuhudiwa kwa muda mrefu kiasi kwamba kumekuwepo uwezekano wa kuibuka makabilianao ya kijeshi baina ya pande mbili katika Bahari Nyeusi na Bahari ya Baltic na pia katika mpaka wa Russia wa Ukraine na mpaka wa Russia na nchi za NATO.

Onyo kali la Putin linaonyesha kuwa Moscow iko tayari kabisa kutoa jibu kali kwa Wamagharibi iwapo mistari yake myekundu itavukwa. Russia inasema nchi za Magharibi na hasa Marekani zitabeba dhima ya makabiliano yoyote yatakayotokea.

 

Tags