May 06, 2021 12:37 UTC
  • Ndege ya kijeshi ya Russia yatimua ndege ya kijasusi ya Marekani

Russia imetangaza leo Alkhamisi kuwa imetumia ndege yake ya kivita kufukuza ndege ya kijasusi ya Marekani iliyokuwa ikijaribu kuingia katika anga ya nchi hiyo kinyume cha sheria katika Bahari ya Chukchi.

Katika taarifa, Kituo cha Usimamizi wa Ulinzi wa Kitaifa cha Russia kimesema Moscow imetumia ndege ya kijeshi aina ya MiG-31 kuifukuza ndege hiyo ya kijasusi ya Marekani iliyokuwa ikielekea kuingia katika anga ya Russia.

Shirika la habari la TASS limenukuu taarifa hiyo ikieleza kuwa: Marubani wa ndege ya kijeshi ya Russia waligundua ndege ya kistratejia ya Marekani aina ya RC-135 ikielekea katika anga ya Russia lakini ikaisindikiza juu ya Bahari ya Chukchi.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, ndege hiyo ya kijasusi ya US hata hivyo iligunduliwa na kutimuliwa kabla ya kuhujumu anga ya Russia.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kituo cha Usimamizi wa Ulinzi wa Kitaifa cha Russia, ndege ya kivita ya Russia aina ya MiG-31 imerejea salama katika kambi yake, baada ya kufanya operesheni hiyo kwa kufuata sheria za kimataifa za anga.

Ndege ya kijasusi ya Marekani aina ya RC-135

Russia imekuwa ikilalamikia mara kwa mara kitendo cha kichokozi cha ndege za kivita na kijasusi za Marekani na Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) kuruka karibu na mpaka wake wa Magharibi.

Chokochoko hizo zilishadidi kuanzia mwaka 2014, baada ya eneo la Crimea lililokuwa likimilikiwa na Ukraine kujiunga na Russia, kufuatia kura ya maoni ya kuainisha mustakabali wa eneo hilo, na pia baada ya kuibuka makabiliano ya kijeshi mashariki mwa Ukraine.

 

 

 

Tags