May 09, 2021 02:11 UTC

Baada ya Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya maarufu kwa jina la Brexit, sasa hivi matunda na matokeo mabaya ya kujitoa huko yameanza kuonekana katika nyuga mbalimbali.

Kwa vile huko nyuma Uingereza ilikuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya, hakukuwa na tatizo lolote katika kutumia maeneo ya baharini ya nchi wanachama wa umoja huo zikiwemo shughuli za uvuvi. Hata hivyo hali hivi sasa imebadilika kikamilifu.

Baada ya kuongezeka mzozo baina ya Uingereza na Ufaransa kuhusu haki ya uvuvi katika bandari kuu ya kisiwa cha Jersey yaani bandari ya Saint Helier, sasa Paris nayo baada ya London, imetuma manuwari zake za kijeshi kwenye eneo hilo.

Ufaransa inasema kuwa imetuma manuwari zake za kijeshi kwenye eneo hili kwa ajili ya kupiga doria na kulinda usalama wa wakazi wa eneo hilo.

Kisiwa cha Jersey chenye mzozo mkubwa baina ya Uingereza na Ufaransa

 

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya London kutangaza kuwa imeamua kutuma manuwari mbili za jeshi la kifalme kwenda kusimamia na kudhibiti jaribio lolote la kuzingirwa kisiwa hicho.

Ufaransa imetangaza wazi kuwa haibabaishwi na kikosi cha majini cha ufalme wa Uingereza. Kisiwa cha Jersey kiko katika mfereji wa Manche. Kina ukubwa wa kilomita mraba 116 na kiko karibu na fukwe za Normandy, nchini Ufaransa.

Kisiwa cha Jersey ni mali ya Uingereza lakini si sehemu ya nchi ya Uingereza. Hata hivyo serikali ya Uingereza inasema kuwa kwa mujibu wa sheria za nchi hiiyo, ina wajibu wa kulinda usalama wa kisiwa hicho na kukiwakilisha kimataifa.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson, anasema kuwa, ni haki ya raia wa Uingereza kuvua samaki katika kisiwa hicho. Hata hivyo hivi karibuni serikali ya Ufaransa ilitoa onyo kali kwamba itakata umeme wa kisiwa cha Jersey. Umeme wote wa kisiwa cha Jersey unatokea Ufaransa kwani kiko umbali wa kilomita 20 tu kutoka nchini Ufaransa. 

Si hayo tu, lakini pia Paris imetishia kuchukua hatua kali dhidi ya Uingereza baada ya London kuweka sheria mpya za kurahisishia boti za Uingereza kufanya shughuli za uvuvi katika kisiwa cha Jersey na kuwabana raia wa Ufaransa.

Sheria mpya za uvuvi zilizowekwa na utawala wa ndani wa kisiwa cha Jersey zimezingatia makubaliano mapya baina ya Uingereza na Umoja wa Ulaya baada ya London kujitoa kwenye umoja huo. Sheria hizo zinapingwa na Ufaransa.

Brexit imesababisha na itaendelea kusababisha mizozo mingi baina ya Uingereza na Umoja wa Ulaya

 

Kwa mujibu wa sheria hizo mpya, kuanzia sasa wavuvi wa Ufaransa watalazimika kuwa na vibali maalumu vya kufanya shughuli za uvuvi kwenye eneo hilo. Vibali hivyo lazima vithibitishe kwamba kabla ya hapo pia Wafaransa hao walikuwa wanafanya shughuli za uvuvi kwenye maji ya kisiwa hicho.

Ufaransa inasema, sheria hizo mpya zilizotungwa na Uingereza, zimeongeza mambo ambayo hayamo katika makubaliano ya huko nyuma. Wakuu wa Ufaransa nao wametangaza kuwa, hakuna hatua zozote za kiufundi zilizowasilishwa kwa Umoja wa Ulaya kuhusu shughuli za uvuvi katika eneo hilo, hivyo sheria hizo mpya za Uingereza hazina itibari yoyote kwa Ufaransa. 

Licha ya kuweko makubaliano maalumu baina ya Uingereza na Umoja wa Ulaya baada ya Brexit, lakini tangu mwanzo ilikuwa inajulikana wazi kwamba kutazuka mizozo mingi baina ya pande hizo mbili na halitokuwa jambo rahisi kuepuko mizozo hiyo.

Ukiachilia mbali mizozo ya mipaka ya ardhini baina ya Umoja wa Ulaya na Uingereza ambapo pande hizo mbili zina mpaka mmoja tu wa ardhini uliopo baina ya Uingereza na Ireland Kaskazini na hadi sasa mzozo huo wa mpaka wa ardhini bado haujatatuliwa kutokana na utata na ugumu wake mkubwa, kuna mizozo mikubwa zaidi pia katika mipaka ya majini baina ya Uingereza na nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na katika suala la uvuvi na shughuli za baharini. 

Javad Kachueian, mtaalamu wa masuala ya Ulaya anasema, kitendo cha Uingereza cha kujitoa katika Umoja wa Ulaya kitasababisha matatizo mengi kwa nchi hiyo na kwa Umoja wa Ulaya kiujumla. Mizozo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ya muda mfupi na muda mrefu baina ya pande mbili, ni sehemu ya matunda na matokeo mabaya ya kitendo hicho cha Uingereza cha kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya.

Tags