May 09, 2021 13:24 UTC
  • Mapya yaibuliwa kuhusu jinai ya kigaidi ya Marekani ya kumuua shahidi Kamanda Qassem Suleimani

Tovuti ya habari ya Yahoo News imetoa ripoti ya taarifa mpya kuhusu operesheni ya jinai ya kinyama iliyofanywa na jeshi la kigaidi la Marekani ya kumuua shahidi aliyekuwa kamanda wa kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Luteni Jenerali Qassem Suleimani.

Ripoti hiyo ya Yahoo News imeashiria mashirikiano yaliyokuwepo baina ya magaidi Wamarekani na utawala wa Kizayuni wa Israel na kueleza kwamba, operesheni hiyo itaathiri hali ya kistratejia ya serikali ya sasa ya Marekani inayoongozwa na Joe Boiden katika eneo la Asia Magharibi katika kipindi cha miaka ijayo.

Katika sehemu nyingine ya ripoti hiyo ambayo imewanukuu maafisa waandamizi wa zamani wa shirika la ujasusi la Marekani CIA imeelezwa kuwa, katika kipindi cha miaka kadhaa nyuma, shirika hilo na lile la usalama wa taifa la Marekani yalitumia dola milioni mia kadhaa katika miradi ya utafiti ili kufuatilia shughuli za vifaa vya elektroniki na vyombo vya mawasiliano vya Wairani na kudukua na kunasa mazungumzo na mawasiliano aliyokuwa akifanya kamanda shahidi Qasem Suleimani. Hata hivyo maafisa hao hawakufafanua kama gharama hizo kubwa za fedha zilizotumika ziliwezesha kufikiwa lengo lililokusudiwa au la.

Mike Pompeo (kulia) na Brian Hook

Yahoo News imewanukuu maafisa waandamizi wa zamani au wastaafu katika wizara ya mambo ya nje ya Marekani wakieleza kuhusu hatua za usalama ilizochukua Washington kwa ajili ya viongozi wake kwa kuhofia kisasi ambacho Iran ingelipiza na kuongeza kuwa, hatua za usalama kwa baadhi ya viongozi hao zilichukuliwa kimya kimya na kwamba katika bajeti ambayo Trump aliisaini katika siku za mwishoni mwa mwaka uliopita, aliidhinisha matumizi ya dola milioni 15 kwa ajili ya watu wanaokbailiwa na kitisho kikubwa cha dola la kigeni au maajenti wake.

Sehemu ya mwisho ya ripoti hiyo imeeleza kuwa, Marekani inahofia zaidi Iran kulipiza kisasi dhidi ya aliyekuwa waziri wake wa mambo ya nje Mike Pompeo na mjumbe maalumu wa nchi hiyo masuala ya Iran Brian Hook.

Luteni Jenerali Qassem Suleimani, kamanda wa kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ambaye mnamo Januari 3, 2020 alielekea Iraq kwa mwaliko rasmi wa viongozi wa nchi hiyo, aliuawa shahidi katika shambulio la kigaidi la anga lililofanywa na jeshi vamizi na la kigaidi la Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad.../