May 10, 2021 01:34 UTC
  • Mwaka wa tatu wa Marekani kujitoa katika mapatano ya JCPOA, juhudi nyingi zisizo na maana

Miaka mitatu iliyopita, Mei 8 2018, Donald Trump rais wa zamani wa Marekani aliiondoa rasmi nchi hiyo katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia mashuhuri kama JCPOA, kwa madai kwamba yalikuwa mapatano mabaya zaidi kuwahi kufikiwa katika historia ya nchi hiyo.

Baada ya hapo serikali yake alikataa kutekeleza ahadi zake katika mapatano hayo yaliyofikiwa na kuidhinishwa kimataifa kupitia azimio 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Licha ya kuwepo ukosoaji na upinzani mkali wa jamii ya kimataifa dhidi ya hatua hiyo, lakini Trump alikataa kulegeza msimamo na kuamua kuiwekea Iran vikwazo vikali zaidi vya kiuchumi katika fremu ya kile kilichotajwa kuwa ni mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi ya serikali ya Washington dhidi ya Tehran, na wakati huo huo kupinga mapango wowote wa kuyaokoa mapatano hayo.

Wakati huo serikali ya Trump ilidai kuwa ingeilazimisha Tehran kusalimu amri na hatimaye kuipigia magoti baada ya kukubali kutekeleza masharti 12 yaliyotangazwa mwaka huo huo wa 2018 na Mike Pompeo, waziri wake wa mambo ya nje. Pompeo alitoa arodha ya masharti hayo ambayo eti yalipaswa kutekelezwa na Tehran kabla ya kufanyika mazungumzo ya pande mbili, suala ambalo bila shaka lilikejeliwa na kuchukuliwa kuwa kichekesho na wachambuzi wengi na vile vile yombo vya habari. Baadhi ya Masharti hayo yaliitaka Iran isimamishe mara moja mpango wake wa nyuklia na uundaji makombora na vile vile ipunguze ushawishi wake kieneo.

Mike Pompeo

Kwa maneno mengine ni kwamba Trump aliitaka Iran isalimu amri na kujidhalilisha moja kwa moja mbele ya Marekani. Alidhani kwamba kupitia vikwazo na mashinikizo ya kiwango cha juu angeweza kuilazimisha Iran iketi na serikali yake kwenye meza ya mazungumzo kwa lengo la kubadilisha mapatano ya JCPOA kwa maslahi ya serikali ya Washington. Pamoja na mashinikizo hayo yote lakini mwishowe Trump alidhalilika kwa kufukuzwa madarakani na kulazimika kuondoka White House tarehe 20 Januari mwaka huu bila kufikia ndoto na lengo lake hilo la kijuba, kama ilivyokiri wazi mmoja wa waliokuwa na misimamo mikali zaidi katika serikali yake dhidi ya Iran ambaye si mwingine bali ni John Bolton, mshauri wa zamani wa usalama wa taifa wa Marekani.

Trump alikosolewa vikali kwa kutokuwa na stratijia maalumu kuhusu Iran, kuanzisha migogoro na mivutano isiyo na maana na Tehran na wakati huo huo kuwatenga washirika muhimu wa Marekani barani Ulaya. Kusimama imara taifa la Iran nkabala wa vikwazo na mashinikizo hayo ya Washington hatimaye kuliupelekea utawala wa Trump kukata tamaa na mwishowe kushindwa kufikia malengo yake dhidi ya mfumo wa Kiislamu wa Iran.

Hili ni jambo ambalo wanalikiri weledi na viongozi wengi wa kisiasa, ndani na nje ya Marekani. Mikhail Ulyanov, mwakilishi wa Russia katika mashirika ya kimatraifa yaliyo na makao makuu yao mjini Vienna Austria  amesema kwamba matokeo ya Marekani kujitoa katika mapatano ya JCPOA hayakuwa mengine bali ni kushindwa na kufedheheka hadharani, na sasa inajaribu kujirudishia heshima iliyopotea kupitia mazungumzo ya Vienna.

Serikali ya Trump licha ya kufukuzwa uongozini lakini ingali inakosolewa vikali kutokana na siasa zake zisizo na muelekeo kuhusu Iran na pia kushindwa vikwazo na mashinikizo ya kiwango cha juu dhidi ya Tehran. Chris Murphy Seneta wa chama cha Democrat ameandika katika ujumbe wake wa Twitter kwamba: Kumbukeni kwamba Marekani haikupata faida yoyote kutokana na vikwazo vya Trump dhidi ya Iran.... Vikwazo hivyo havikuwa na taathira yoyote.

Chris Murphy

Katika kampeni zake za uchaguzi wa  Septemba 2020, Joe Biden, Rais wa sasa wa Marekani alisema kuwa Trump alifanya kosa kubwa kuitoa Marekani katika mapatano ya JCPOA, jambo ambalo alisema lilikwenda kinyume na maslahi ya Marekani na kuitenga nchi hiyo katika ngazi za kimataifa. Pamoja na hayo lakini rais huyo hajachukua hatua yoyote ya maana kwa ajili ya kurekebisha hali hiyo na badala yake anaendeleza tu siasa zile zile za Trump za vikwazo na mashinikizo dhidi ya Tehran. Bila kuashiria ni nani aliyejitoa katika mapatano ya JCPOA na kukataa kutekeleza majukumu yake, ameitaka Iran itekeleze ahadi zake kwanza kabla nayo kuamua kurejea katika mapatano hayo.

Huku akithibitisha kwamba Marekani ingali inatekeleza siasa zile zile za Trump za vikwazo na mashinikizo ya juu  dhidi ya Iran, Joseph Cirincione, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Marekani amesema kwamba iwapo Biden haitabadilisha siasa zake dhidi ya Iran kuna hatari kubwa ya kusambaratika mazungumzo muhimu ya JCPOA.

Katika kukabiliana na siasa hizo zisizo za kimantiki za Biden Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza wazi kuwa itaanza tena kutekeleza ahadi zake za mapatano ya JCPOA pale tu Marekani itakapoamua kuondoa kivitendo na sio kwa maneno matupu, vikwazo vyote ilivyoweka dhidi ya Tehran na baada ya Iran kuhakikisha kuwa kweli vikwazo hivyo vimeondolewa.

 

Tags