May 10, 2021 12:02 UTC
  • Jeshi la Ufaransa latahadharisha kuhusu uwezekano wa kutokea vita vya ndani

Mamia ya wanajeshi wa Ufaransa wameandika tena barua ya wazi wakitahadharisha kuhusu uwezekano wa kutokea vita vya ndani na uasi wa kiraia nchini humo.

Tahadhari hiyo imetolewa baada ya majenerali wa jeshi la Ufaransa kutoa barua ya wazi wakitahadharisha kuhusu uwezekano wa kutokea mgawanyiko na vita vya ndani. 

Jarida la Ufaransa la Le Point limeripoti kuwa: Baada ya barua iliyoandikwa tarehe 21 Aprili na majenerali wa jeshi la Ufaransa, kwa mara nyingine tena wanajeshi elfu mbili wa nchi hiyo wamewaandikia barua maafisa wa serikali ya Paris akiwemo Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, mawaziri na wabunge wa nchi hiyo.

Wanajeshi hao wamesema kunashuhudiwa machafuko katika miji na vijiji vya Ufaransa na kwamba, sera za migawanyiko ya kimakundi zinatawala anga ya nchi huku propaganda chafu zikiendelea kuwa jambo la kawaida. 

Ufaransa inazongwa na migogoro ya ndani

Barua hiyo imetahadharisha kuwa, kuna hatari ya kusambaratika nchi hiyo ambayo inazongwa na migogoro na kwamba, kinyume na inavyosemwa, hali hiyo ya mchafukoge na machafuko, haitasababisha mapinduzi ya kijeshi, bali itafuatiwa na uasi wa kijamii. 

Katika barua ya kwanza iliyoandikwa tarehe 21, majenerali wastaafu 20 wa jeshi la Ufaransa, karibu maafisa mia moja wa ngazi za juu na zaidi ya wanajeshi elfu moja waliandika barua ya wazi wakitahadharisha kuhusu uwezekano wa kugawanywa nchi hiyo na kutokea vita vya ndani. 

Uchunguzi wa maoni uliofanyika karibuni unaonesha kuwa, wananchi waliowengi wa Ufaransa wanaafikiana na barua ya majenerali wastaafu na maafisa wa jeshi waliotahadharisha kuhusu uwezekano wa kutokea mapinduzi na kujitosa uwanjani jeshi la nchi hiyo kwa ajili ya kudhibiti hali ya mambo.