May 11, 2021 13:10 UTC
  • Maiti za wagonjwa wa corona zatoswa kwenye Mto Ganga nchini India

Baadhi ya vyombo vya habari vya India vimeripoti kuwa viwiliwili vya watu waliofariki kwa ugonjwa wa Covid-19 nchini humo vimeonekana vikielea kwenye Mto mkubwa wa Ganga wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa gazeti la The Times of India, maiti kadhaa za wagonjwa wa corona zimeonekana zikielea kwenye fukwe za mto huo katika maeneo ya mji wa Buxar ulioko kwenye mpaka wa majimbo mawili masikini ya India ya Bihar na Uttar Pradesh.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, tukio hilo la karibuni linadhihirisha ukubwa wa kiwango cha usambaaji wa virusi vya corona na maambukizi ya ugonjwa wa covid-19 hadi kwenye maeneo ya mbali ya India.

Times of India limeongeza kuwa, kutupwa maiti za ugonjwa wa Covid-19 kwenye mto wa Ganga ni ishara ya kukosekana suhula za kutosha na zinazohitajika kwa ajili ya shughuli za mazishi katika maeneo hayo.

Wakazi wenyewe wa maeneo hayo wameeleza kwamba, kuonekana maiti zikielea katika mto huo itakuwa kumesababishwa na kufurika maeneo ya kuchomea maiti au hali duni ya maisha ya familia za watu hao za kutoweza kumudu gharama za kuni za kuchomea wapendwa wao.

Ashok Kumar, afisa wa eneo hilo la Buxar amethibitisha kupatikana miili 40 iliyokuwa ikielea kwenye kingo za mto Ganga, lakini baadhi ya vyombo vya habari vimesema, idadi ya miili hiyo inafika hata 100.  

Viongozi wa upinzani nchini India wanasema, kupatikana kwa maiti hizo ni ushahidi wa kutosajiliwa idadi halisi ya vifo vinavyosababishwa na ugonjwa wa Covid-19.

Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa karibu watu 4,000 wanafariki dunia kila siku kwa ugonjwa wa Covid-19 nchini India huku idadi ya vifo ikiwa imefika watu laki mbili na nusu.../

Tags