May 11, 2021 17:12 UTC
  • Hua Chunying
    Hua Chunying

China imepinga unafiki wa Merekani katika madai yake ya kutetea haki za Waislamu waliowachache katika eneo la Magharibi mwa China la Xinjiang, na kusisitiza kuwa, Marekani imeua Waislamu wengi katika vita na operesheni zake za kijeshi kuliko nchi nyingine yoyote duniani.

Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa Twitter Jumanne ya leo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya China alielezea rekodi mbaya ya Marekani ya ukiukaji wake wa haki za binadamu duniani na akasema, kikao kilichopngwa kufanyika mjini New York ambacho kitajadili haki za Waislamu huko Xinjiang, kinafanyika ili kuwapotosha walimwengu kuhusu ukweli wa mambo.

Hua Chunying amesema: "Badhi ya watu nchini Marekani wananunua mashahidi na wataalamu wachache wa uwongo, lakini wanakataa kusikiliza sauti zinazozidi zile za wasema uwongo, na wala hawatilii maanani wito wa Wachina bilioni 1.4, wakiwemo zaidi ya watu milioni 25 wa makabila yote ya mkoa wa Xijiang.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya China amesema Marekani imeuawa Waislamu wengi zaidi kuliko nchi yoyote duniani na kuongeza kuwa, nchi hiyo imeanzisha vita na operesheni za kijeshi katika nchi zaidi ya 80 duniani kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na imeua zaidi ya watu laki nanne mbali na kuwalazimisha makumi ya mamilioni ya raia wa Iraq, Syria na Afghanistan kuwa wakimbizi.

Marekani imeua maelfu ya Waislamu Afghanistan

Wawakilishi wa kudumu wa Marekani, Uingereza na Ujerumani katika Umoja wa Mataifa (UN) kesho Jumatano wamepangwa kuhutubia kikao kitakachojadili jinsi umoja huo na nchi wanachama wake wanaweza kutetea haki za binadamu za wakazi wa mkoa wa Xinjiang.

China inakanusha vikali madai kwamba, inakiuka haki za waliowachache katika mkoa huo.

Akizungumza na waandishi wa habari, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya China amekemea jaribio la Marekani la kuandaa kikao hicho akiitaja hatua hiyo kuwa ni "matusi na kebehi" na akasema, wafadhili wake wanakusudia kutumia "masuala ya haki za binadamu kama wenzo wa kisiasa wa kuingilia mambo ya ndani ya China."

Waislamu wa Uighur huko Xinjiang wanaunda karibu asilimia 45 ya wakazi wa eneo hilo. Nchi za Magharibi zinaituhumu Beijing kuwa inafanya ubaguzi wa kitamaduni, kidini, na kiuchumi katika eneo hilo.

Mwaka jana, jopo la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa lilidai kwamba, Waislamu milioni mbili wa jamii ya Uighurs wamelazimishwa kuishi katika "kambi za kisiasa za kubadili itikadi zao" katika eneo hilo lenye mamlaka ya ndani.

Tags