May 12, 2021 00:44 UTC
  • Kupasishwa marufuku ya hijabu kwa wafanyakazi wa serikali katika Bunge la Ujerumani

Baraza la Juu la Bunge la Ujerumani (Bundesrat) limepasisha sheria inayowapiga marufuku wafanyakazi wa serikali na polisi kuvaa vazi la hijabu.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, kuvaa nembo za kiadiolojia au kidini katika sehemu za kazi ni marufuku. Licha ya kuwa kidhahiri sheria hiyo iko katika sura jumla na haijaashiria waumini na wafuasi wa dini fulani, lakini kivitendo sheria hii inawalenga wanawake wa Kiislamu wanaofanya kazi katika idara za serikali nchini Ujerumani.

Kwa mujibu wa sheria hiyo ambayo kishahiri imewaanisha wafanyakzi wa serikali na jeshi la polisi ni kuwa, maafisa wa serikali na polisi hawaruhusiwi kuvaa hijabu wakiwa katika maeneo ya kazi. Uamuzi huu uliopasishwa na Baraza la Juu la Bunge la Ujerumani (Bundesrat) umekabiliwa na ukosoaji mkubwa wa asasi na jumuiya za Kiislamu na hata baadhi ya maafisa wa serikali za majimbo nchini Ujerumani. Immanuel Hoff, mmoja wa viongozi wa jimbo la Thuringen anasema: Kuweka sheria kama hii katika jamii kutazusha matatizo.

Afisa huyo ambaye ni mwakilishi katika Baraza la Juu la Bunge la Ujerumani sambamba na kuashiria kwamba, kutekelezwa sheria hiyo kunaweza kuleta vizuzi kwa wanawake Waislamu wanaofanya kazi katika idara za serikali amesisitiza kuwa, kutekelezwa sheria hii kutaibua mashtaka kwa Mahakama ya Katiba.

Maandamano ya kuunga mkono uvaaji hijabu

 

Ukweli wa mambo ni kuwa, sheria hii inakinzana wazi kabisa na katiba ya Ujerumani ambayo inatambua uhuru wa dini na hiari ya mtu kuchagua kazi kwa wafanyakazi wa serikali.

Suala la chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) na njama za kukabiliana na nembo za Kiislamu na madhihirisho yake hususan hijabu ya wanawake wa Kiislamu barani Ulaya ikiwemo Ujerumani limegeuka na kuwa jambo linalokuwa na kuchukua wigo mpana siku baada ya siku. Moja ya mambo hasasi katika mataifa ya Ulaya ikiwemo Ujerumani ni kadhia ya hijabu ya Kiislamu hususan kwa harakati na vyama vya mrengo wa kulia vyenye kufurutu ada ambavyo katika miaka ya hivi karibuni vimekuwa katika mkondo wa kukua na kupata nguvu nchini Ujerumani.

Hii ni katika hali ambayo, Waislamu ni moja ya jamii inayoishi nchini Ujerumani ambayo haiwezekani kuifumbia macho. Jamii hii imekuwa ikitaka kuheshimiwa sheria za Kiislamu ikiwemo hijabu kwa wanawake wa Kiislamu. Kwa muktadha huo, kupasishwa hivi karibuni katika Baraza la Juu la Bunge la Ujerumani (Bundesrat) sheria inayopiga marufuku uvaaji hijabu ni njama inayolenga kuwabana wanawake wa Kiislamu na kuwalazimisha wachague baina ya kazi au kuvaa hijabu.

Maandamano ya kupinga chuki dhidi ya Uislamu

 

Takwimu za hivi karibuni za Idara ya Wahajiri na Wakimbizi nchini Ujerumani zinaonyesha kuwa, takribani Waislamu milioni 5.3 hadi milioni 5.6 wanaishi katika nchi hiyo ya bara Ulaya. Idadi hii ni sawa na asilimia 6.4 hadi 6.7 ya wakazi wote wa Ujerumani.

Mintarafu hiyo, kuna idadi ya kuzingatiwa ya wanawake wa Kiislamu wanaoishi katika nchi hiyo ambapo kwa kuzingatia takwa la akthari yao la kuvaa na kujistiri na hijabu, sasa wamejikuta wakikabiliwa na mbinyo na kizuizi kikubwa. Hii ni katika hali ambayo, vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya wanawake nchini Ujerumani vimechukua mkondo mpana katika miaka ya hivi karibuni.

Burhan Kesici, Mkuu wa Baraza la Waislamu nchini Ujerumani anasema: Wanawake wanaojistiri kwa vazi la hijabu wamekuwa katika hatari zaidi ya kukabiliwa na mashambulio na hujuma za chuki dhidi ya Uislamu. Nukta ya kuzingatiwa ni hii kwamba, hatua ya hivi karibuni ya Baraza la Juu la Bunge la Ujerumani (Bundesrat) imekuja baada ya hatua ya Bunge la Seneti la Ufaransa inayowawekea vizuzi na mipaka wanawake na mabinti wa Kiislamu kuhusiana na uvaaji wa hijabu.

Matukuo mhaya yanaonyesha kuwa, kuna mipango na mikakati maalum iliyoandaliwa huko barani Ulaya ya kushadidisha chuki dhidi ya Uislamu na kuongeza mashinikizo dhidi ya Waislamu. Vyama vya mrengo wa kulia vyenye misimamo ya kufurutu ada na wanasiasa wanaojali fikra za umma katika nchi za Ulaya ikiwemo Ujerumani kama chama cha mrengo wa kulia chenye misimamo ya kufurutu ada cha Alternative for Germany (AfD), ambacho kikiwa na lengo la kuwavutia wapiga kura, kimeongeza hujuma zake dhidi ya Waislamu na kuwataja Waislamu kama wasababishaji wa ugaidi, uhaba wa ajira na ukosefu wa usalama katika nchi hiyo.

Polisi mwanamke aliyevaa hijabu nchini Scotland

 

Wafuasi wa chama hiki wenye misimamo ya kufurutu ada wamekuwa mstari wa mbele katika kueneza vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya Waislamu.

Vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na kushambuliwa Waislamu kwa maneno na hata kupigwa sambamba na ubaguzi na kushadidi mashinikizo dhidi yao likiwemo suala la kupigwa marufuku hijabu ni mambo ambayo yameongezeka nchini Ujerumani. Katika miaka ya 2019 na 2020 Waislamu na vituo vya Uislamu nchini Ujerumani vililengwa mara 950 na 901 mtawalia. 

Misimamo na utendaji wa asasi za serikali kama Bunge katika nchi za Ulaya kama Ujerumani na Ufaransa, nao umekuwa katika mkondo wa kuongeza mashinikizo na kueneza chuki dhidi ya Waislamu. Kwa muktadha huo, mwenendo unaochukua mkondo wa kuongezeka wa chuki dhidi ya Uislamu na kuionyesha dini ya Uislamu kuwa ni tishio huko Ulaya, ni hatua ambazo zimezifanya jamii za Waislamu zilizoko katika nchi hizo ziishi katika mazingira magumu. Hali hii imekuwa ikuchukua mkondo mpana zaidi siku baada ya siku.

Tags