May 12, 2021 00:53 UTC
  • Russia: Marekani inaendelea kuongeza kiwango cha silaha zake za vijidudu

Katibu wa Baraza la Usalama la Russia amesema: Marekani imejikita katika kupanua uzalishaji wa silaha zake za biolojia inazokusudia kuzitumia dhidi ya nchi tofauti duniani.

Nikolai Patrushev ametangaza kuwa, katika miaka ya karibuni Marekani na waitifaki wake wameongeza kwa kiwango kikubwa tafiti za kibiolojia katika  nchi nyingi duniani. Patrushev ameongeza kuwa, ana wasiwasi kutokana na hatua hizo zinazochukuliwa na Marekani na waitifaki wake katika mipaka ya Russia, akisema zinaweza kuwa hatarishi, kwa sababu vijidudu angamizi vya maabara za Marekani na shirika la kijeshi la NATO zilizoko karibu na mipaka ya Russia vinaweza kwa bahati mbaya vikasambaa angani na kuhatarisha maisha ya watu wengi.

Wakati huohuo, Vladimir Jabbarov, naibu mkuu wa kamati ya masuala ya kimataifa ya baraza la shirikisho (Seneti) la Russia amesema, popote pale wanapokuwepo Wamarekani, hali ya uthabiti huvurugika na akaongeza kuwa, "uwezekano wa kujengwa vituo vya kijeshi vya Marekani katika nchi za Asia ya Kati nao pia utakuwa na taathira hasi kwa hali ya eneo hilo."

Siku ya Jumatatu, gazeti la Wall Street Journal liliripoti kuwa, baada ya kuwaondoa askari wake nchini Afghanistan, huenda Marekani ikawapeleka askari hao katika nchi za Asia ya Kati hususan Uzbekistan.../