May 13, 2021 02:14 UTC
  • Mbunge wa Ulaya: Israel inafanya jinai kwa kuungwa mkono na Marekani na Ulaya

Mbunge mmoja wa Ireland katika Bunge la Ulaya amesema kuwa mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi madhlumu na wasio na ulinzi wa Palestina ni mauaji ya kizazi na kwamba, jinai hizo zisingelifanywa na Wazayuni kama si uungaji mkono wa pande zote wa Marekani na Ulaya kwa Israel.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Mbunge Mick Wallace akisema hayo kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, mtu yeyote mwenye akili timamu anastaajabishwa na uungaji mkono wa Umoja wa Ulaya kwa jinai za kivita za Israel dhidi ya wananchi wa Palestina. Amesema, mtu yeyote atakayekaa kimya bila ya kulaani jinai za Wazayuni wauaji, wenye nyoyo za jiwe na wabaguzi, basi ni bora mtu huyo aendelee kuwa bubu milele. 

Mapigano yameongezeka katika mpaka wa Ukanda wa Ghaza huko Palestina kutokana na utawala wa Kizayuni wa Israel kufanya ukatili na jinai kubwa dhidi ya Wapalestina wa Quds na ndani ya Msikiti wa al Aqsa ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu.

Ukombozi wa Quds ni ahadi ya Mwenyezi Mungu ambayo lazima itatimia

 

Hadi tunaandika habari hii, utawala dhalimu na katili wa Kizayuni ulikuwa umeshaua shahidi Wapalestina wasipungua 30 katika mashambulio yake ya anga na mizinga dhidi ya Ukanda wa Ghaza uliozingirwa kila upande. Watoto wadogo 10 ni miongoni mwa Wapalestina wauliouliwa shahidi na Wazayuni katika mashambulizi hayo.

Kila mwenye hisia ya kibinadamu analaani jinai hizo za Wazayuni katika kona zote za dunia. Nchi mbalimbali, taasisi za kimataifa na mashirika ya haki za binadamu, nayo yanaendelea kulaani jinai hizo za kutisha za Israel.

Hadi tunaandaa habari hii nchi nyingi za Kiislamu na Kiarabu zilikuwa tayari zimelaani ukatili wa wanajeshi wa Israel na kutaka hatua zichukuliwe kimataifa kukabiliana na jinai hizo za wavamizi wa Quds.

Tags