May 13, 2021 02:52 UTC
  • Makazi ya raia wa Palestina yanashambuliwa na jeshi la Israel
    Makazi ya raia wa Palestina yanashambuliwa na jeshi la Israel

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imetahadharisha kuhusu uwezekano wa kufanyika tena jinai za kivita katika mashambulizi ya sasa ya Israel dhidi ya watu wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Taarifa iliyotolewa na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai yenye makao yake makuu nchini Uholanzi, Fatou Bensouda imeeleza wasiwasi wake kuhusu ongezeko la machafuko katika Ukingo wa Magharibi na maeneo mengine ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kutahadharisha kuwa, kuna uwezekano utawala wa Kizayuni wa Israel ukakari jinai za kivita huko Palestina.

Machafuko ya sasa katika ardhi za Palestina yalianza baada ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kuvamia na kuvunjia heshima Msikiti wa al Aqsa na raia wa Wapalestina mji wa Quds. Wanajeshi katili wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamewahujumu Waislamu waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala ndani ya Msikiti wa al Aqsa na raia wengine wa Palestina. Israel pia imekuwa ikishambulia vikali mji wa Gaza na hadi sasa makumi ya raia wa Palestina wameuawa kwa mshambulizi ya ndege za kivita za utawala huo haramu.

Mashambulizi ya ndege za kivita za Israel dhidi ya makazi ya raia, Gaza

Mashambulizi hayo ya kinyama ya Israel yamejibiwa kwa makombora na maroketi ya wanamapambano wa Palestina yaliyovurumishwa dhidi ya miji ya utawala huo haramu ukiwemo mji mkuu, Tel Aviv. 

Taarifa ya Wizara ya Afya ya katika eneo la Ukanda wa Gaza inasema kuwa, raia wasiopungua 69 wa Kipalestina wameuawa shahidi hadi jana katika mashambulizi ya jeshi la Israel na wengine 388 wamejeruhiwa. 17 kati ya mashahidi hao ni watoto wadoto na 7 ni wanawake.