May 13, 2021 07:32 UTC
  • Jopo la wataalamu: Ulimwengu ungeweza kuzuia janga la COVID-19

Jopo la kujitegemea limetangaza kuwa, wimbi kubwa la janga la corona lingeweza kuzuiwa lakini "ukosefu wa maamuzi thabiti" na "uratibu duni" vilipelekea kupuuzwa kwa ishara na tahadhari zilizotolewa.

Katika ripoti yake ya mwisho iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu ambayo ilitolewa jana Jumatano, jopo huru la IPPPR limesema, mlolongo wa maamuzi mabaya umepelekea kuaga dunia watu wasiopungua milioni 3.3 kutokana na ugonjwa wa COVID-19 hadi sasa na kuharibu uchumi wa dunia.

Ripoti ya IPPPR imesema: Taasisi mbalimbali zilishindwa kulinda watu, na viongozi wanaopinga sayansi waliharibu imani ya umma katika suala la kuchukua hatua za kulinda afya. Imesema hazikuchukuliwa hatua za haraka za kukabiliana na mlipuko wa virusi vya corona vilivyogunduliwa kwa mara ya kwanza huko Wuhan, Uchina mnamo Disemba 2019 na kwamba nchi mbalimbali hazikutilia maanani tahadhari ya hatari ya virusi hivyo.

Maiti za wahanga wa corona zikichomwa moto, India

Jopo hilo limezitaka nchi tajiri zaidi kuchangia dozi bilioni moja za chanjo ya corona kwa nchi masikini ili kukabiliana na janga la sasa. Vilevile limeyataka mataifa tajiri zaidi ulimwenguni kufadhili mashirika mapya yaliyojitolea kujiandaa na janga lijalo.

Ripoti ya jopo la IPPPR imetayarishwa kwa wito wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Jopo hilo limeongozwa kwa pamoja na Waziri Mkuu wa zamani wa New Zealand Helen Clark na rais wa zamani wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel ya 2011.

Tags