May 14, 2021 09:40 UTC

Viongozi wa Ufaransa wanaendelea kuchukua hatua za kuipiga vita waziwazi dini tukufu ya Kiislamu. Hatua ya karibuni kabisa ni ya kupigwa marufuku Muislamu wa kike asijiandikishe kugombea katika uchaguzi kutokana na Hijab yake.

Chama kipya cha LREM kilichoasisiwa na rais wa hivi sasa wa Ufaransa, Emmanuel Macron kimedai kuwa, kwa mujibu wa sera za chama chake hicho na katika nchi ya kisekula kama Ufaransa, watu wenye misimamo ya kidini hawana nafasi katika kampeni za uchaguzi.

Hatua ya hivi sasa ya chama hicho cha Macron imechukuliwa katika hali ambayo, wimbi la kunyanyaswa na kukandamizwa Waislamu limetanda katika kila kona ya Ufaransa na kwenye sehemu mbalimbali za Ulaya.

Katika kipindi cha miezi kadhaa sasa, Emmanuel Macron amekuwa akichukua misimamo ya kipumbavu na isiyoingia akilini na hafichi chuki zake dhidi ya Waislamu kila kinapotokezea kisingizio kidogo tu. Miongoni mwa chuki za wazi kabisa za Macron na serikali yake dhidi ya Waislamu wa Ufaransa, ni kuunga mkono kwake majarida, vyombo vya habari na wahuni wanaotoa matusi dhidi ya Uislamu na matukufu yake, kuweka sheria kali za kuwaminya na kuwanyanyasa Waislamu na pia kupiga vita waziwazi, vazi la staha ya mwanamke wa Kiislamu, Hijab, kama vile kuwapiga marufuku ya kuvaa Hijab watoto wa Kiislamu wenye umri wa chini ya miaka 18.

Waislamu Ufaransa katika maandamano ya kulaani unyanyasaji wanaofanyiwa

 

Muda wote Macron anasema, anachojali yeye ni kulinda mfumo unaopinga dini wa kisekula. Lakini anaposema dini, Macron na watawala wa nchi nyingine za Magharibi na wenzao kama wao, huwa wanakusudia dini ya Kiislamu. Ukandamizaji mkubwa wanaofanyiwa Waislamu wa maeneo tofauti duniani kwa madai ya kulinda mfumo wa kisekula unaotawala katika nchi hizo, ni ushahidi wa wazi wa uhakika huo. Macron anadai anapigania mfumo wa kisekula unaochukia dini, lakini vitendo vyake kimsingi vinawalenga moja kwa moja Waislamu na hafichi kusema kuwa, Waislamu wanaoshikamana na mafundisho ya dini yao, na wanawake wa Kiislamu wanaojistahi na kujisitiri vizuri, hawana nafasi katika utamaduni wa Ufaransa. 

Sasa hivi ukandamizaji wa Waislamu umeongezeka kupindukia nchini Ufaransa. Macron anajificha kwenye chaka la kukabiliana na Waislamu kutokana na kufeli vibaya katika kuendesha nchi na hasa katika suala zima la uchumi. Ahadi alizotoa wakati wa kampeni za uchagizi ameshindwa kuzitimiza, mgogoro wa ukosefu wa kazi nchini Ufaransa ni mkubwa, janga la corona na kushindwa Macron kulisimamia vizuri ni sehemu ndogo tu ya malalamiko mengi yanayomwandama rais huyo anayewachukia Waislamu. Uchunguzi wa maoni unaonesha kuwa, umaarufu wa Macron unazidi kuporomoka siku baada ya siku.

Wataalamu wa mambo wanasema kuwa, lengo la Macron la kuwanyanyasa Waislamu wa Ufaransa ni katika kujitafutia umaarufu kabla ya uchaguzi. Wanasema, Macron anataka muda wote awemo kwenye vyombo vya habari. Viongozi wa Ufaransa wanawashambulia bila ya huruma Waislamu wakidai kuwa eti ndio wanaosababisha matatizo kama ya ugaidi, ukosefu wa kazi na ukosefu wa amani baada ya kushindwa kutekeleza ahadi zao kwa wananchi wa Ufaransa.

Waislamu ni jamii inayonyanyaswa sana barani Ulaya

 

Siasa hizo zimekuwepo kwa muda mrefu barani Ulaya. Cha kushangaza ni kuwa, viongozi hao wa Ulaya wanaelekeza mashambulizi yao bila ya huruma dhidi ya dini tukufu ya Kiislamu, wakati ni wao ndio wanaoweka tawala vibaraka katika nchi za Waislamu, ni wao ndio wanaounda magenge ya kigaidi katika ulimwengu wa Kiislamu, ni wao ndio ambao wanaanzisha tawala za kigaidi kama utawala wa Kizayuni wa Israel unaofanya jinai zisizo na kifani dhidi ya Waislamu na watu wasio na hatia. Waislamu ndio wahanga wakuu wa ugaidi unaofanywa na watu waliolelewa, kusomeshwa na kupewa mafunzo ya kijeshi na misimamo mikali barani Ulaya. Sasa kichekesho ni kuwa, hizo hizo nchi za Ulaya zinailaumu dini tukufu ya Kiislamu na kuihusisha na vitendo viovu vinavyofanywa na watu hao hao waliolelewa na kusomeshwa na viongozi hao hao wa Ulaya.

Tumalizie kwa kunukuu maneno ya mbunge wa Uingereza, Afzal Khan ambaye amegusia ripoti ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na kusema kuwa, dhana mbaya, ubaguzi na chuki za wazi dhidi ya Waislamu zinaelekea kuwa janga kubwa hivi sasa duniani. Amesema, wasiwasi wetu ni kwamba Ufaransa imeingia kwenye mkondo hatari sana na inaendelea kuisukuma mbali jamii ya Waislamu.

Tags