May 15, 2021 09:56 UTC
  • Upinzani wa Ujerumani na Ufaransa wa kufanyika maandamano dhidi ya Israel; nembo ya uungaji mkono wa Magharibi kwa jinai za Wazayuni

Baada ya kuwaka moto wa vita na mapigano baina ya utawala haramu wa Israel na Wapalestina katika siku za hivi karibuni, madola ya Magharibi yamefumbia macho kabisa jinai za Tel-Aviv hususan hujuma na mashambulio ya anga na kulishambulia kwa mabomu eneo la Ukanda wa Gaza.

Madola hayo badala yake yamelaani hatua ya makundi ya kijihadi ya Palestina ya kurusha makombora huko Israel ambako kunafanyika katika fremu ya kujibu uchokozi na jinai za Wazayuni dhidi ya Wapalestina. Baadhi ya madola ya Ulaya yakiwa upande wa Israel yametangaza rasmi kupiga marufuku katika nchi zao maandamano dhidi ya utawala dhalimu wa Israel.

Licha ya utawala haramu wa Israel kufanya mashambulio ya kinyama dhidi ya ukanda wa Gaza hivi karibuni, lakini Steffen Seibert, msemaji wa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, ametahadharisha kwamba, serikali ya Ujerumani haiwezi kabisa kuvumilia suala la kufanyika maandamano dhidi ya Israel katika ardhi ya nchi hiyo. Steffen Seibert ametetea jinai za Israel na kueleza kwamba, hatua hizo zinafanyika kwa ajili ya kujihami. Aidha amesema kuwa, Israel ina haki ya kujihami na kujitetea na mshambulio inayokabiliwa nayo.

Jumatano iliyopita, serikali ya Ujerumani ililaani mashambulio ya maroketi ya wanamapambano wa Palestina huko Gaza ambayo ni majibu ya uvamizi wa Israel na kudai kwamba, mashambulio hayo ya maroketi hayawezi kuhalalishika.

Wananchi wqa Kenya wakiandamana kuwaunga mkono Wapalestina

 

Serikali ya Ufaransa nayo imefuata mkumbo wa Ujerumani wa kupiga marufuku maandamano ya wananchi katika nchi yake ya kuwaunga mkono Wapalestina. Serikali ya Ufaransa imetangaza kupiga marufuku maandamano ya kuwaunga mkono Wapalestina yaliyokuwa yafanyike Jumamosi ya leo.

Gérald Darmanin, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa akitoa radiamali yake kwa wito wa kufanyika maandamano leo Jumamosi kuwaunga mkono wananchi wa Palestina aliandika ujumbe katika ukurasa wake wa mtandao wa kijami wa Twitter kwamba: Nimemtaka Mkuu wa Polisi mjini Paris apige marufuku maandamano yaliyokuwa yafanyike leo kuhusiana na mzozo wa hivi karibuni huko Asia Magharibi baina ya Israel na Wapalestina.

Polisi ya Paris ilitoa taarifa mapema leo ya kupiga marufuku maandamano hayo.

Wakilalamikia hatua hiyo ya serikali ya Ufaransa ya kuegemea upande mmoja na ya kuwaunga mkono Wazayuni, watumijia wa mitandao ya kijamii katika nchi hiyo ya bara Ulaya wamesisitiza kuwa, wataandamana kulalamikia ukoloni na  jinai dhidi ya binadamu na ubaguzi aina ya apartheid na ukandamizaji" wa Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.

Agnes Calamard, Katibu Mkuu wa Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International

 

Kuweko miito ya kufanyika maandamano katika nchi za Ulaya ni jambo ambalo limekuwa na umuhimu maradufu hasa kwa kuzingatia mashambulio ambayo hayajawahi kushuhudiwa ya Israel dhidi ya watu wa Palestina na kuongezeka idadi ya mashahidi na majeruhi wa mashambulio hayo huko Palestina.

Agnes Calamard, Katibu Mkuu wa Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International amezungumzia tishio la Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel la kutekeleza mashambulio zaidi dhidi ya Ukanda wa Gaza ambapo sambamba na kukumbusha takwimu za mashahidi hadi sasa huko Palestina amesema: Katika hatua ya awali, raia wa kawaida ndio wanaolipa gharama ya mashambulio hayo.

Katika msimamo wake wa kidhahiri mwanzoni mwa kuanza vurugu na machafuko baina ya Israel na Wapalestina huko Quds Mashariki na hususan katika Msikiti wa al-Aqswa, Umoja wa Ulaya ulitoa taarifa ya kukemea vurugu hizo na kuzitaja kuwa hazikubaliki. Aidha ulitoa wito wa kuchukuliwa hatua za kupunguza hali hiyo tete kama ambavyo ulitangaza kupinga hatua ya kufukuzwa Wapalestiina kutoka katika eneo la Sheikh Jarrah.

Wanamapambano wa Kipalestina wameendelea kkujibu uchokozi wa Israel kwa kuvurumisha makombora

 

Hata hivyo, hivi sasa Umoja wa Ulaya umevua ngozi ya kondoo na kuonyesha sura yake halisi ya mnyama katili kutokana na kuwaunga mkono Wazayuni maghasibu na wakati huo huo kulaani waziwazi mashambulio ya makombora ya wanamapambano wa Kipalestin ambayo kimsingi ni ya kujihami na kujitetea baada ya kushambuliwa.

Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya akizungumza kwa njia ya simu na Gabi Ashkenazi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Israel alisisitiza uungaji mkono wa umoja huo kwa utawala huo unaotenda jinai.

Kwa muktadha huo, madola ya Ulaya na Umoja wa Ulaya zimeonyesha kuwa, kama ilivyo Marekani daima zimekuwa zikichukua misimamo ya wazi ya kuuunga mkono bila masharti utawala dhalimu wa Israel na huu ni undumakuwili wa wazi kwa madola hayo yanayodai kuwa vinara wa kutetea haki za binadamu duniani.

Tags