May 17, 2021 03:35 UTC
  • Asasi za Kiislamu Marekani zasusia dhifa ya Idi White House kulalamikia uungaji mkono wa Washington kwa jinai za Israel

Jumuiya na asasi za Kiislamu nchini Marekani zimesusa kuhudhuria dhifa ya kila mwaka ya Idul-Fitri inayoandaliwa na Ikulu ya White House kulalamikia uungaji mkono wa serikali ya nchi hiyo kwa jinai za kinyama za utawala haramu wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wakiwemo wa Ukanda wa Gaza.

Jumuiya hizo, likiwemo Baraza la Mahusiano ya Marekani na Uislamu CAIR, zimeeleza katika taarifa kwamba zimeamua kususia dhifa ya Idi iliyofanyika jana Jumapili Ikulu ya White House kwa sababu ya Washington kuunga mkono mashambulio ya kinyama ya utawala wa Kizayuni dhidi ya ardhi za Palestina ukiwemo Ukanda wa Gaza na kusisitiza kuwa hatua hiyo ya Marekani haikubaliki.

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imeeleza kwamba, ikiwa White House itaendelea kufuata njia isiyokubalika na iliyo dhidi ya maadili ya kuunga mkono mashambulio ya kinyama ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina; na wanawake na watoto wengi zaidi huko Palestina wakaendelea kuuawa shahidi kwa mashambulio ya utawala ghasibu wa Kizayuni, mahusiano ya serikali ya Marekani na Baraza la Mahusiano ya Marekani na Uislamu CAIR, asasi zingine za kiraia na za kutetea haki za binadamu nchini humo yataharibika vibaya sana.

Jinai za Israel dhidi ya raia Wapalestina, wakiwemo hata watoto wadogo

Kwa siku ya nane sasa jeshi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel linafanya mashambulio ya kinyama dhidi ya eneo la Ukanda wa Gaza, ambapo ripoti za karibuni kabisa zinaeleza kwamba Wapalestina wanaokaribia 200 wameshauwa shahidi hadi sasa wakiwemo watoto 58 na wanawake 34.

Ripoti kutoka Gaza zinasema, Wapalestina 42 waliuawa shahidi katika hujuma za jana tu Jumapili za jeshi la utawala dhalimu wa Kizayuni, makumi ya wengine walijeruhiwa na majengo mawili ya makazi ya raia yalibomolewa kikamilifu.

Hayo yanajiri katika hali ambayo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilifanya kikao hapo jana kuzungumzia hali ya Gaza lakini lilishindwa kutoa hata taarifa tu ya pamoja ya kuonyesha kutiwa wasiwasi na kinachojiri katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.../ 

 

Tags