May 22, 2021 02:28 UTC
  • Serikali ya Biden yatakiwa iushinikize utawala wa Saudia uondoe mzingiro dhidi ya Yemen

Maseneta kadhaa nchini Marekani wamemuandikia barua Rais Joe Biden wa Marekani na kumtaka aishinikize Saudi Arabia ili iondoe mzingiro dhidi ya Yemen. Waliotia saini mapatano hayo ni maseneta Elizabeth Warren na Bernie Sanders.

Katika barua yao maseneta hao wamesema mzingiro wa muungano unaoongozwa na Saudia dhidi ya Yemen umezuia misaada ya chakula dawa na bidhaa nyingine muhimu kuwafikia watu wa Yemen.

Sehemu ya barua hiyo inasema: "Tunataka utumie ushawishi wako wote na nyenzo kama vile kusimamisha kwa muda mikataba ya uuzaji silaha na ushirikiano wa kijeshi na baada ya hapo uiamuru Saudia isitishe haraka na bila masharti mzingiro wake dhidi ya Yemen."

Punde baada ya kuingia madarakani, serikali ya Biden ilitakiwa na Umoja wa Mataifa pamoja na taasisi zingine za kimataifa na pia wajumbe katika Bunge la Kongres ichukue hatua za kubatilisha uamuzi wa serikali ya Donald Trump wa kuitangaza harakati ya Ansarullah ya Yemen kuwa eti ni kundi la kigaidi. Uazumuzi huo wa Trump uliandamana na kuiwekea harakati hiyo vikwazo. Kimsingi Biden ametakiwa kubadilisha muelekeo wa sera za Marekani kuhusu vita vya Yemen.

Wakati wa kampeni zake za uchaguzi, Biden alitoa nara dhidi ya Saudi Arabia na akavitaja vita dhidi ya Yemen kuwa ni 'maafa ya kistratijia' huku akidadi kuwa angehitimisha uungaji mkono wa Marekani kwa oparesheni za kijeshi dhidi ya Yemen sambamba na kusitisha uuzaji silaha kwa muungano huo.

Biden

Pamoja na hayo, baada ya kuingia Ikulu ya White House, Biden aliitaja Saudia kuwa mshirika wa karibu wa Saudia. Serikali ya Biden kidhahiri imekuwa ikitekeleza sera zinazotofuatiana na za Trump katika vita vya Yemen na kwa msingi huo Februari 2021 ilitangaza kuiondoa harakati ya Ansarullah katika makundi ya kigaidi.

Katika hatua nyingine, Washington pia imetangaza kusitisha kwa muuda uuzaji wa silaha za kuhujumu kwa Saudia na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Pamoja na hayo hatua hizo hazijaweza kuathiri vita vinavyoendeshwa na muungano wa Saudia dhidi ya watu madhulumu wa Yemen na hivi sasa muungano huo ungali unaendeleza mashambulizi ya anga kila siku dhidi ya Wayemen.

Vita hivyo vinaendelezwa sambamba na muungano huo wa Saudia kutekeleza mzingiro wa nchi kavu, baharini na angani dhidi ya Yemen. Serikali ya Biden pia imesisitiza kuendelea kuunga mkono Saudi Arabia kijeshi katika kukabiliana na kile kinachotajwa kuwa ni tishio kutoka nje.

Mnamo Machi 2015 Saudi Arabia, kwa kushirikiana na Imarati na kwa uungaji mkono wa serikali ya Obama, ilianzisha hujuma ya pande zote dhidi ya watu madhulumu wa Yemen ambao nchi yao ni masikini zaidi katika bara Arabu.

Vita hivyo vilianzishwa kwa lengo la kumrejesha madarakani Abdu Rabuh Mansour Hadi, ambaye alijiuzulu kama rais wa Yemen na kukimbilia Riyadh. Kimsingi vita hivyo vilianzishwa ili kueneza satwa ya Saudia nchini Yemen na kupora utajiri wa nchi hiyo.

Taasisi zinazofungamana na Umoja wa Mataifa kwa mara kadhaa zimeonya kuhusu athari mbaya zinazotokana na kuendelea hujuma ya muungano vamizi wa Saudia dhidi ya Yemen, na hivyo kupelekea watu wa Yemen kukumbwa na maafa makubwa ya kibinaadamu ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika karne hii.

Chris Murphy, seneta wa chama cha Democrat katika ukurasa wake wa Twitter ameandika kuwa: "Vita vya Yemen vimepelekea kuibuka maafa makubwa zaidi ya kibinadamu hivi saa. Watoto milioni mbili wanakabiliwa na mauti kutokana na njaa nchini humo."

Pamoja na kuwepo hali hiyo mbaya,  lakini serikali ya Biden haijachukua hatua yoyote ya maana kuzishinikiza  Saudia na Imarati ili zisitishe mzingiro wao dhidi ya Yemen na hata katika hali hiyo mbaya Washington imewawekea vikwazo maafisa kadhaa wa kijeshi wa Yemen.

Watoto ni waathirika wakuu wa vita vya Saudia dhidi ya Yemen

 

Tim Lenderking,   mjumbe maalumu wa Marekani katika masuala ya Yemen Alhamisi alitangaza kuwekewa vikwazo makamanda wawili wa Jeshi la Yemen na kamati za wananchi nchini humo.

Alidai kuwa kumechukuliwa hatua za kusitisha mzingiro dhidi ya viwanja vya ndege na bandari za Yemen ili kuwafikishia Wayemen misaada ya dharura lakini muungano vamizi wa Saudia haujachukua hatua za kivitendo kuondoa mzingiro uliopo.

Maafisa hao wa kijeshi wa Yemen wanawekewa vikwazo wakati ambao serikali ya Marekani imefumbia macho hujuma za kinyama za Saudia dhidi ya watu madhulumu wa Yemen.

Tags