May 27, 2021 02:19 UTC
  • Baraza la Haki za Binadamu la UN leo linajadili mpango wa kuundwa tume ya kuchunguza jinai za Israel dhidi ya Wapalestina

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limepokea muswada unaotaka kuundwa tume ya kimataifa itakayochunguza jinai na uhalifu uliofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya raia wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.

Kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kinachofanyika leo Alkhamisi kimeitishwa na Pakistan, ikiwakilisha nchi wanachama katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), na serikali ya Palestina.

Muswada uliowasilishwa na nchi hizo mbili umetaka kuundwe tume ya kimataifa itakayochunguza ukiukaji wote wa haki za binadamu uliofanyika katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina ikiweno Quds Mashariki tangu tarehe 13 mwezi Aprili.

Vilevile umetaka kuchunguzwa sababu zote zilizoibua mzozo wa sasa na ukosefu wa usalama ikiwa ni pamoja na vitendo vya ubaguzi na ukandamizaji unaofanyika kwa msingi wa kaumu, mbari au dini.

Uchunguzi huo pia utaainisha wahusika wa jinai na uhalifu huo na kuwafikisha mahakamani ili kukomwesha mtindo wa wahalifu kukwepa mkono wa sheria.

Wapalestina wasiopungua 253 wakiwemo watoto wadogo 66 waliuawa shashidi katika mashambulizi ya utawala haramu wa Israel yaliyoanza tarehe 10 hadi 21 mwezi huu wa Mei.

Ijumaa iliyopita wataalamu 10 wa kimataifa katika masuala ya haki za binadamu waliitaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ifanye uchunguzi kuhusu mashambulizi ya kinyama yaliyofanywa na Israel dhidi ya raia na vilevile uharibifu mkubwa uliofanywa na jeshi na ndege za kivita za utawala huo katika Ukanda wa Gaza.

Wataalamu hao wa kimataifa walisisitiza kuwa, operesheni ya jeshi la Israel ya kuwafukuza kwa mabavu Wapalestina wa kitongoji cha Sheikh Jarrah na Silwan (Silvan) katika eneo la Quds Mashariki ndiyo cheche iliyoanzisha moto wa vita vya karibuni baina na Wapalestina na utawala ghasibu wa Israel.  

Israeli ina mpango wa kuwafukuza karibu Wapalestina 300 wanaoishi katika nyumba 14 za eneo hilo na kuyakabidhi makazi yao ya jadi kwa walozi wa Kiyahudi.

Tags