May 31, 2021 02:36 UTC
  • Kupungua kupindukia akiba ya fedha za kigeni nchini Uturuki

Licha ya serikali ya Rais Recep Tayyip Edrogan kuchukua hatua nyingi za kuimarisha uchumi na kuongeza pato la kigeni, lakini pole pole uchumi wa nchi hiyo umeingia kwenye mgogoro mkubwa zaidi na kila siku idadi ya wananchi wa Uturuki wanaoingia kwenye orodha ya watu maskini, inaongezeka.

Hayo yameelezwa na duru rasmi za Uturuki. Benki Kuu ya nchi hiyo imetoa ripoti na kusema: Akiba ya fedha za kigeni ya Uturuki ilifikia dola bilioni 46.2 mwishoni mwa mwezi Aprili 2021 kiwango ambacho kimeshuka kwa asilimia 12.9 ikilinganishwa na mwezi wa kabla yake wa Machi.

Kuporomoka thamani ya sarafu ya fedha ya taifa ya Uturuki ambako kumeandaa mazingira ya kupanda mfumuko wa bei, kuongezeka ukosefu wa kazi na kushuhudiwa nakisi ya bajeti, kumeishia kwenye kuongezeka umaskini kwa wananchi wa nchi hiyo na sasa hilo limekuwa ni moja ya migogoro mikubwa inayokabiliana nayo serikali ya Uturuki katika kipindi cha miaka mitano sasa.

Ukweli ni kuwa siasa zisizo sahihi za kifedha zilizofuatwa na serikali na wakuu wa masuala ya kiuchumi hasa rais mwenyewe wa Uturuki ndiko kulikosababisha kutokea matatizo ya hivi sasa ya kupungua kwa kiwango kikubwa akiba ya fedha za kigeni huko Uturuki.

Wapinzani wa Erdogan wanamlaumu kwa siasa mbovu zilizoutia kwenye matatizo makubwa uchumi wa Uturuki

 

Wimbi la janga la COVID-19 na kujiingiza serikali ya Erdogan katika mizozo ya kijeshi kwenye maeneo mbalimbali duniani hasa Syria, Libya na Azerbaijan, kumeitumbukiza Uturuki katika mgogoro mkubwa wa ukosefu wa kazi unaotokana na kupungua kasi harakati za maeneo ya ukuzaji uchumi. Hiyo imetajwa kuwa ni moja ya sababu za kuongezeka umaskini siku baada ya siku kati ya wananchi wa Uturuki.

Kuporomoka sekta ya utalii ambayo ilikuwa inaandaa nafasi nyingi za ajira huko Uturuki kutokana na kuenea kirusi cha corona na kupelekea wimbi kubwa la wananchi wa Uturuki wanaofanya kazi ndogo ndogo wapoteze kazi na kipato chao, ni sababu nyingine iliyoitumbukiza Uturuki kwenye mgogoro wa hivi sasa wa kupungua mno akiba ya fedha za kigeni.

Abdülmenaf Kıran, mmoja wa wataalamu wa Uturuki anazungumzia athari mbaya za kiuchumi zilizosababishwa na ugonjwa wa COVID-19 nchini humo akisema: 

Suala la kufungwa nchi nzima ya Uturuki ni tofauti na kufungwa nchi nzima ya China na nchi nyingine duniani. Kwa kweli Uturuki haiwezi kuchukua hatua ya kufunga nchi nzima. Na sababu yake ni kuwa, jengo na msingi wa uchumi wa Uturuki ni tete sana na unaathirika vibaya na haraka. Serikali ya Erdogan nayo haina uwezo wa kustahamili mashinikizo yote ya jamii ya kuhitajia msaada mkubwa wa fedha kutoka serikalini.

Alaakullihaal, inabidi tuseme kuwa, mgogoro wa kifedha ulioikumba serikali ya Uturuki hivi sasa na matatizo ya kiuchumi ya wananchi wa nchi hiyo, si kitu kilichoanzia muda mfupi nyuma.

Siasa za Uturuki za kuingilia kijeshi maeneo mengine kama Syria, Libya na Azerbaijan zimetajwa kuwa ni sababu ya kupungua vibaya akiba ya fedha za kigeni ya nchi hiyo

 

Miaka kadhaa iliyopita, wakati Uturuki ilipokumbwa na mgogoro wa fedha za kigeni na kuporomoka vibaya thamani ya Lira, sarafu ya nchi hiyo, Benki Kuu ya Uturuki ililazimika kumimina kiwango kikubwa cha fedha za kigeni katika soko la nchi hiyo. Hata hivyo hatua hiyo haikuisaidia sana serikali ya Uturuki na matokeo yake ni kuwa kiwango kikubwa cha akiba ya fedha za kigeni za nchi hiyo kilimegwa na kupotea gizani.

Hatua ya Rais Recep Tayyip Erdogan ya kubadilisha mara kadhaa magavana wa benki kuu, kiliwakasirisha washika dau wengi katika uchumi wa nchi hiyo na hivyo kuikwamisha Benki Kuu kudhibiti mfumuko wa bei, ilishindwa kuzuia kuporomoka thamani ya sarafu ya nchi hiyo kama ambavyo haikuweza pia kulirejesha soko la fedha za kigeni la Uturuki katika hali yake ya ustawi.

Uchunguzi wa kiutaalamu uliofanywa na taasisi rasmi za Uturuki unaonesha kuwa mamilioni ya wananchi wa nchi hiyo hivi sasa wana maisha magumu. Taasisi rasmi za serikali ya Uturuki zinasema kuwa, mstari wa umaskini nchini Uturuki ni wa kipato cha Lira 2,830 kwa siku wakati taasisi zisizo rasmi zinasema kuwa, kila familia ya watu wanne nchini Uturuki, inahitajia kwa uchache Lira 9,000 kuweza kumudu kiwango cha chini kabisa cha maisha yake kila siku.

Tags