Jun 03, 2021 02:31 UTC
  • Biden atahadharisha kuhusu ugaidi wa wabaguzi wa rangi nchini Marekani

Katika hotuba yake ya juzi kwenye kumbukumbu ya mwaka wa 100 tangu baada ya mauaji yaliyofanywa na wazungu dhidi ya Wamarekani weusi katika mji wa Tulsa jimboni Oklahoma, Rais Joe Biden wa Marekani aliutaja ugaidi wa wazungu wabaguzi wa rangi wanaojiona kuwa bora kuliko wanadamu wengine kuwa ni tishio hatari zaidi kwa Marekani.

Biden ambaye anakuwa rais wa kwanza wa Marekani kutembelea eneo la mauaji ya umati ya mamia ya raia weusi wa nchi hiyo katika mji wa Tulsa yaliyofanyika miaka mia moja iliyopita, ameonya juu ya kuendelea kuwepo fikra za ubaguzi wa rangi nchini Marekani. 

Amesema: "Hatuwezi kupata makimbilio salama kutokana na chuki za kimbari. Hii leo ugaidi wa wazungu wanaojiona kuwa bora zaidi ya wanadamu wengine ndiyo tishio kubwa zaidi dhidi ya nchi yetu, na wala si kundi la Daesh au al Qaida; bali ni makundi ya wabaguzi wa kizungu."

Tarehe 31 hadi Mosi Mei mwaka 1921 wazungu wa Marekani waliopewa silaha za moto na maafisa wa serikali walishambulia makazi ya raia weusi katika wilaya ya Greenwood, mji wa Tulsa katika jimbo la Oklahoma na kuuwa watu zaidi 300 na kuacha wengine 10,000 wakiwa bila ya makazi. Wazungu hao walifanya uharibu mkubwa na kusawazisha kabisa mji huo na ardhi baada ya kuteketeza kila kitu. Mji huo wa Wamarekani weusi ulikuwa umestawi na kupiga hatua kubwa za maendeleo kiasi cha kujulikana kwa jina la Black Wall Street. Mashambulizi ya wabaguzi hao yalihaibu kabisa maduka makubwa ya biashara, maktaba, mahospitali, shule na kadhalika.

Talsa baada ya mauaji ya wazungu dhidi ya Wamarekani weusi

Hadi sasa hakuna hata manusura mmoja au familia ya wahanga wa mauaji ya umati ya Tulsa aliyepewa fidia kutokana na uhalifu huo wa kutisha, na makampuni ya bima ya Marekani yamekataa katakata kushugulikia kesi hiyo. 

Ubaguzi wa rangi na ukatili wa kimfumo nchini Marekani daima vimekuwa vikitajwa kuwa miongoni mwa sifa kuu za jamii ya Marekani tangu nchi hiyo ilipoundwa mwaka 1776. Licha ya mapambano ya miaka mingi ya Wamarekani weusi ya kupigania haki zao za kiraia lakini hadi sasa sehemu hiyo ya jamii ya Marekani ingali inasumbuliwa na ubaguzi wa aina mbalimbali. Wamarekani hao wenye asili ya Afrika wakati mmoja walikuwa wahanga wa mauaji yaliyopewa jina la "lynch' yaliyotekelezwa kwa mtu mweusi kukamatwa na kundi la wazungu kisha kutundikwa na kungongwa au mauaji ya umati kama yale yaliyofanyika katika mji wa Greenwood huko Oklahoma mwaka 1921. 

Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa juu kabisa wa Marekani kumulika uhalifu na ukatili huo wa kutisha uliokuwa ukifanywa na wazungu wabaguzi wa rangi dhidi ya raia wenye asili ya Afrika wa nchi hiyo.  Katika hotuba yake iliyosikilizwa pia na manusura watatu tu wa mauaji ya umati ya Tulsa ambao wana umri wa zaidi ya miaka mia moja, Biden amesema: "Tunazungumzia tukio lililojiri miaka mia moja iliyopita, na mimi ni rais wa kwanza wa Marekani kuja Tulsa. Nimekuja hapa kusaidia jitihada za kuvunja kimya, kwa sababu jeraha linapanuka zaidi katika kumya". Vilevile amewataka Wamarekani kufanya jitihada za kung'oa mizizi ya ubaguzi wa rangi wa kimfumo katika maeneo yote ya nchi hiyo. 

Wamarekanu wenye asili ya Afrika ndiyo jamii ya pili kwa ukubwa nchini Marekani baada ya Walatino, na wanaunda karibu asilimia 14 ya jamii yote ya Marekani. 
Baada ya kuchaguliwa Barack Obama kuwa rais wa kwanza mweusi nchini Marekani kuanzia 2009 hadi 2017 ilitarajiwa kwamba, hali ya jamii ya Wamarekani weusi ingeboreka kidogo. Hata hivyo jamii hiyo imeendelea kusumbuliwa na hali mbaya zaidi ya kiuchumi na kijamii siku baada ya nyingine. 

Japokuwa harakati ya kupigania haki za kiraia za Wamarekani weusi ilizusha wimbi kubwa katika njia ya kutetea haki za sehemu hiyo ya jamii ya Marekani katika muongo wa 1950, lakini hali ya sasa ya Marekani inaonesha kuwa, ubauzi wa rangi, ukandamizaji, manyanyaso na dhulma za kijamii zingali zinawaandama watu wa tabaka hulo.
Takwimu zinaonesha kuwa, Wamarekani weusi ndio wanaotiwa nguvuni na kufungwa jela zaidi ya mbari nyingine. Vilevile raia hao wenye asili ya Afrika ndio wanaouliwa zaidi kwa kupigwa risasi mara kwa mara na maafisa wa polisi. 

Jamii ya Wamarekani weusi inakabiliana na ubaguzi na manyanyaso ya polisi, ukatili wa makundi ya wazungu wenye misimamo mikali ya kibaguzi, ukosefu wa usawa wa kiuchumi na masharti mapya ya upigaji kura katika baadhi ya majimbo ya Marekani ambayo wakosoaji wanasema yanalenga kuwazuia wapigakura weusi na malatino ili kupunguza ushawishi wao katika chaguzi za nchi hiyo.
Haya yote yanathibitisha zaidi kauli ya rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama aliyesema: Ubaguzi wa rangi umo katika vinasaba vya Wamarekani. 

Kukiri kwa Rais Joe Biden kwamba, ugaidi wa wabaguzi wa kizungu wanaojiona bora zaidi ya wanadamu wengine ndio tishio kubwa zaidi nchini humo, ni ishara kwamba, jamii ya Marekani inakabiliana na changamoto kubwa ya kiusalama na kijamii katika karne hii ya 21 

Tags