Jun 06, 2021 02:37 UTC
  • Vikwazo vya Marekani kipindi cha corona ni ukiukaji wa haki za binadamu

Wimbi la maambukizi ya virusi vya corona linaendelea kuchukua roho za watu katika nchi mbalimbali duniani huku jumuiya za kimataifa zikisisitiza udharura wa kutolewa chanjo ya kukabiliana na virusi hivyo na kusambazwa chanjo hiyo na vifaa vingine vya tiba ili kufanikisha jitihada za kuvuka kipindi cha sasa cha janga hilo la kimataifa.

Hata hivyo vikwazo vya kiuchumi vya Marekani dhidi ya nchi na mataifa mbalimbali ya dunia vinaendelea kuwa kizingiti kinachozuia kupelekwa chanjo na vifaa vya tiba na dawa kwa baadhi ya nchi.

Katika uwanja huo wawakilishi wa nchi mbalimbali katika Umoja wa Mataifa wanasema kuwa, vikwazo hivyo vya Marekani vimekuwa na taathira hasi katika mfumo wa tiba na huduma za mtibabu wa kimataifa hususan katika nchi ambazo zimeathiriwa sana na maambukizi ya corona. Wawakilishi hao walikutana jana na kusema kuwa, vikwazo vya kiuchumi vya Marekani vinakiuka haki za binadamu katika kipindi cha maambukizi ya corona kutokana na kuzizuia baadhi ya nchi kupata teknolojia, mifumo na zana za kisasa za tiba na misaada ya kibinadamu inayohitajika katika kipindi cha sasa.

Marekani ndiyo inayoongoza duniani kwa kuziwekea vikwazo nchi nyingine kwa maslahi yake ya kibeberu. Vikwazo hivyo ambavyo vinatekelezwa kwa kutumia visingizio vya aina mbalimbali vya kisiasa yakiwemo madai ya ukiukaji wa haki za binadamu katika nchi kama Russia, China, Iran, Venezuela, Cuba na kadhalika, vimezifanya nchi hizo zishindwe kuingia katika masoko ya kimataifa hata kwa ajili ya kununua dawa na vifaa vya tiba.

Washington imeendeleza sera zake za vikwazo vikali hata katika kipindi cha sasa cha maambukizi ya virusi vya corona ambavyo vimesababisha hali mbaya ya kiuchumi na kitiba kwa nchi zote duniani hususan nchi zinazostawi. Mabadiliko ya uongozi yaliyofanyika huko Marekani na kuja madarakani Joe Biden kama Rais mpya wa nchi hiyo pia havikuwa na taathira yoyote katika sera hizo za ugaidi wa kitiba na kiuchumi wa Marekani. Kutokana na hali hiyo nchi nyingi zimeshindwa kununua au kupata zana na chanjo inayohitajika kwa ajili ya kukabiliana na virusi vya corona. 

Ingawa mashinikizo ya kimataifa yamewalazimisha maafisa wa serikali ya Marekani wadai kuwa, vikwazo vyao havihusu sekta ya chakula na dawa, lakini ukweli ni kwamba, vikwazo hivyo vimeathiri sekta zote. Akizungumzia suala hilo Waziri wa Mashauri ya wa Kigeni wa Iran Muhammad Javad Zarif amesema: Vikwazo vya Marekani ndivyo vibaya na vya kikatili zaidi katika historia ya dunia. Wanasema vikwazo hivyo havihusu chakula na dawa lakini hakuna benki inayoruhusiwa kutuma fedha kwa ajili ya kununua dawa na chakula. Fedha za Iran zimezuiliwa katika benki za kigeni na hatuwezi kutumia fedha zetu sisi wenyewe kununua chakula na dawa."

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Venezuela pia amesema vikwazo vya kiuchumi vya serikali ya Washington vimeizuia Caracas kupata chanjo ya kukabiliana na corona na kuongeza kuwa: "Iwapo fedha za Venezuela zisingezuiliwa nje ya nchi tungeweza kununua mapema dozi milioni thalathini zinazohitajika za chanjo ya corona."

Matatizo na idadi ya vifo vya watu vinavyosababishwa na virusi vya corona bado inaendelea kupanda katika nchi zinazosumbuliwa na vikwazo vya Marekani. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa, raia wa nchi hizo ni wahanga wasio wa moja kwa moja wa vikwazo ambavyo mbali na kuchelewesha na kutatiza juhudi za nchi husika za kupata chanjo ya virusi vya corona, vilevile vinazuia uagizaji wa dawa na vifaa vya tiba na hatimaye kusababisha vifo vya idadi kubwa ya watu.

Kwa sasa idadi kubwa ya watu wanaosumbuliwa na magonjwa maalumu kama saratani, butterfly syndrome (EB) na tiba kemikali wanakabiliwa na hali ngumu sana katika baadhi ya nchi kama Iran, kwa sababu ya vikwazo hivyo vya Marekani. 
Ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa, Alena Douhann anasema: Vikwazo vya Marekni vimekiuka haki nyingi za binadamu katika nchi kama China, Cuba, Haiti, Iran, Nicaragua, Russia, Syria, Venezuela na Zimbabwe.

Marekani na waitifaki wake wamefanya jinai kubwa dhidi ya binadamu kwa kutumia wenzo na fimbo vya vikwazo. Nchi hizo za Magharibi zimefanya jinai dhidi ya binadamu katika nchi nyingi kwa ugaidi wa kitiba licha ya madai yao ya kutetea haki za binadamu. Baya zaidi ni kwamba zinatumia nara na kaulimbiu hiyo hiyo ya kutetea haki za binadamu kuzisulubu nchi mbalimbali licha ya kwamba ndizo wakiukaji wakubwa zaidi wa haki za bindamu. Ukatili uliofanywa na Marekani katika mji wa Tulsa jimboni Oklahoma, maafa yaliyowapata wanafunzi wa shule ya bweni ya Kamloops Indian ya wenyeji asilia wa Canada katika jimbo la British Columbia, mauaji ya kimbari yaliyofanywa na Ujerumani dhidi ya watu wa makabila ya Herero na Nama nchini Namibia na kuhusika Ufaransa katika mauaji ya kimbari ya Rwanda dhidi ya Watutsi ni baadhi tu ya vielelezo vya haki za binadamu za Kimagharibi!     

Tags