Jun 10, 2021 12:58 UTC
  • Kuzabwa kibao Macron, kielelezo cha malalamiko ya wananchi na mgawanyiko wa kisiasa na kijamii Ufaransa

Katika matamshi yake ya kwanza kuhusu safari yake kwenye eneo la Ladrum huko Kusini Mashariki mwa Ufaransa na kuhusu kibao alichozabwa na mtu mmoja ambaye bado hajatambulishwa, Rais Emmanuel Macron amesema, mtu kueleza mitazamo yake ni jambo linalokubalika, lakini ujinga na ukatili havina nafasi katika utawala wa kidemokrasia.

Vyombo vya habari vya Ufaransa vimetangaza kuwa, mtu aliyemzaba kibao Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo ni kijana mwenye umri wa miaka 28. Kijana huyo aliyeonekana kuwa na ndevu nyingi na akiwa amevalia barakoa ya kujikinga na virusi vya corona, alimzaba kibao Rais wa Ufaransa alipokuwa ziarani eneo la Ladrum. Kibao hicho kilikuwa kikali kiasi kwamba, sauti yake inasikika katika mkanda wa filamu ulioonesha tukio hilo. Kijana huyo ambaye alitiwa nguvuni mara moja na walinzi wa Rais wa Ufaransa, anakabiliwa na kifungo cha miaka 3 jela na kulipa faini. Ripoti za vyombo vya habari vya Ufaransa vinasema, kijana huyo alikuwa na mahusiano na kundi lenye misimamo mikali la mrengo wa kulia.

Japokuwa Wafaransa walishawahi kushuhudia mashambulizi kama haya hapo kabla kama shambulizi la keki lililofanywa dhidi ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Nicolas Sarkozy, lakini kuzabwa kibao Rais Macron tena katika kipindi cha mwishoni mwa uongozi wake na kabla ya uchaguzi wa rais wa mwaka ujao, ni dhihirisho la hasira za Wafaransa na kutoridhishwa kwao na utendaji wa kiongozi wao na serikali yake. Tukio hilo pia linadhihirisha mivutano na migawanyiko ya kisiasa na kijamii katika nchi hiyo ya pili kwa ukubwa katika Umoja wa Ulaya. 

Emmanuel Macron

Katika historia ya Ufaransa haijawahi kushuhudiwa Rais wa Jamhuri akizabwa kibao na kudhalilishwa kwa namna hii. Rais wa nchi huko Ufaransa anapewa umuhimu mkubwa kama ilivyokuwa kwa wafalme wa zamani wa nchi hiyo. Shambulizi hilo limelaaniwa na vyama na wanasiasa wote wa Ufaransa ambao wamelitaja kuwa ni sawa na hujuma dhidi ya demokrasia. Ni nadra sana kuweza kushuhudia umoja na mshikamano baina ya vyama na wanasiasa wa mirengo mbalimbali ya Ufaransa kama ilivyokuwa kuhusiana na shambulizi hilo. 

Waziri wa Uchumi wa Ufaransa, Bruno Le Maire amesema harakati hiyo imelivunjia heshima taifa na kutia doa nafasi ya Rais wa Jamhuri. Mwenyekiti wa chama cha Debout la France, Nicolas Dupont-Aignan amesema: "Tukio hili ni kielelezo cha ongezeko linalotia wasiwasi la wimbi na ukatili katika jamii ya Ufaransa. Hili ni shambulizi dhidi ya taifa zima la Ufaransa." 

 Yannick Jadot ambaye ni kiongozi wa Chama cha Kijani na mmoja wa wagombea urais nchini Ufaransa amesema kumshambulia kimwili Rais wa Jamhuri ni sawa na kuishambuli Ufaransa. Jean-Luc Mélenchon ambaye ni miongoni mwa wanasiasa wapenda kiki wa mrengo wa kushoto pia ameeleza mshikamano wake na Emmanuel Macron. 

Si hayo tu, bali hata Marine Le Pen ambaye ni kiongozi wa mrengo wa kulia nchini Ufaransa amelaani shambulio hilo la kuzabwa kibao Emmanuel Macron na akasema, hatua kama hii haikubaliki. 

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wa nchi za Magharibi wanasema, tukio la kuzabwa kibao Emmanuel Macron linatokana na hali tete inayotawala nchini Ufaransa kwa sasa na anga ya ukatili unaoshuhudiwa mara kwa mara nchini humo. Wachambuzi hao wanasema chaguzi za serikali za mitaa zinazotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu na vilevile uchaguzi wa rais wa mwezi Mei mwaka 2022 pia vimechangia katika kushadidi anga ya sasa ya ukosefu wa amani na utulivu nchini humo. 

Pamoja na hayo yote jambo ambalo si rahisi kufichika ni hali ya hasira na kutoridhika Wafaransa na utendaji wa Emmanuel Macron katika nyanja mbalimbali kuanzia mapambano ya serikali yake dhidi ya virusi vya corona hadi katika suala la kushadidi ukatili wa makundi yenye misimamo mikali. Vilevile Wafaransa hawaridhishwi na sera za kiuchumi na kijamii za Macron ambazo zimepekea kuibuka harakati mbalimbali za kijamii kama ile ya Vizibao vya Njano, na vilevile kuongezeka migawanyiko ya kisiasa na kijamii katika nchi hiyo ya Ulaya. 

Hapana shaka yoyote kwamba, kuzabwa kibao Emmanuel Macron ni dhihirisho la kutoridhika Wafarana na hali inayotawala sasa nchini humo.  

Tags