Jun 11, 2021 02:06 UTC
  • Safari ya kwanza ya Joe Biden barani Ulaya, mshikamano wa pande mbili za Atlantic na tahadhari kwa Russia

Rais Joe Biden wa Marekani Jumatano wiki hii aliekelea barani Ulaya ikiwa safari yake ya kwanza nje ya nchi baada ya kushika hatamu za uongozi.

Uingereza ndiyo kituo cha kwanza cha Biden katika safari yake ya kwanza nje ya Marekani. Katika safari hii ya siku 8, Biden anafanya jitihada za kuhuisha uhusiano wa pande mbili za Bahari ya Atlantic uliokumbwa na misukosuko mingi katika kipindi cha utawala wa Donald Trump nchini Marekani. Vilevile anafanya jitihada za kuarifisha upya uhusiano wa nchi yake ya Russia. 

Tangu aliposhika madaraka na kuingia White House na katika matamshi na taarifa zake za mara kwamba, Joe Biden ameashiria hali isiyoridhisha ya uhusiano wa pande mbili za Bahari ya Atlantic kutokana na siasa za mtangulizi wake, Donald Trump, na kuahidi kuhuisha uhusiano huo. Kwa msingi huo inaonekana kuwa, safari ya kwanza ya Biden barani Ulaya katika kipindi cha uongozi wake ni mtihani mkubwa kwa ajili ya kuonyesha uwezo wake wa kidiplomasia katika kusimamia mahusiano ya Marekani na waitifaki wakubwa wa Washington barani Ulaya. Mahusiano hayo yalipigwa na dhoruba nyingi na kuyumbayumba kutokana na siasa za kihasama za Trump, ikiwa ni pamoja na hatua yake ya kuanzisha vita vya ushuru na vita vya kibiashara na nchi za Ulaya, kuiondoa Marekani katika mikataba ya kimataifa kama Mkataba wa Hali ya Hewa wa Paris, makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Mkataba wa Kuzuia Silaha za Nyuklia za Masafa ya Kati (INF) na kuzidisha mashinikizo dhidi ya nchi za Ulaya wanachama wa NATO hususan Ujerumani, akizitaka ziongeze bajeti ya masuala ya kijeshi na mchango wao katika jumuiya hiyo.

Joe Biden na Donald Trump

Awamu ya kwanza ya safari ya Biden itaanza kwa kushiriki katika mkutano wa siku tatu wa viongozi wa G7 katika mji wa pwani wa St Ives huko Cornwall nchini Uingereza. Imepangwa kuwa, agenda ya mkutano huo ni udiplomasia wa chanjo ya corona, biashara, mazingira na ubunifu wa kukarabati miundomsingi katika nchi zinazostawi. Inatazamiwa kuwa Joe Biden atakabiliwa na mashinikizo makubwa yanayoitaka Marekani igawe akiba yake kubwa ya chanjo ya corona inayolimbikizwa katika maghala ya nchi hiyo kwa nchi nyingine zinazohitaji chanjo hiyo. Maafisa wa Marekani pia wanauona mkutano huo kama fursa mwafaka ya kuzishawishi nchi nyingine wanachama wa G7 kwa ajili ya kuchukua misimamo mmoja dhidi ya China.

Baada ya mazungumzo yake na maafisa wa serikali ya London, Biden ataelekea Brusels nchini Ubelgili ambako atafanya mazungumzo na NATO na Umoja wa Ulaya. Inatazamiwa kuwa maudhui kuu ya mazunguzo hayo ni kujadili changamoto zinazosababishwa na Russia na China na kadhia ya wanachama wa jumuiya ya NATO kugharamia zaidi masuala ya kijeshi ya jumuiya hiyo. Kama alivyokuwa Donald Trump, Joe Biden pia anataka nchi wanachama wa NATO ziongeze mchango wao katika bajeti ya shirika hilo la kijeshi la nchi za Magharibi. Kwa kutilia maanani kwamba, awamu ya mwisho ya safari ya Biden barani Ulaya itakuwa kukutana na Rais Vladimir Putin wa Russia, kiongozi huyo wa Marekani atatumia mazungumzo yake ya wanachama wa NATO kama ujumbe na tahadhari kali kwa Putin na sera za serikali ya Moscow katika masuala mbalimbali ya kimataifa. Hasa ikitiliwa maanani kwamba, masuala ya hujuma za mtandaoni na udukuzi dhidi ya taasisi za serikali na zisizo za serikali huko Marekani vimezidisha wasiwasi huko Washington.

Biden na Putin

Uhusiano wa Marekani na Russia katika kipindi hiki cha utawala wa Joe Biden umekumbwa na misukosuko mingi. Tangu aliposhika madaraka, Biden ambaye ana mitazamo iliyodhidi ya Russia amezidisha hujuma na hatua za kihasama dhidi ya Moscow kwa kutumia visingizio vya aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na madai kwamba, Russia iliingilia zoezi la uchaguzi wa rais nchini Marekani. Mtaalamu wa siasa za Magharibi, Ian Bremmer anaamini kwamba: "uhusiano wa Marekani na Russia katika kipini cha utawala wa Biden yumkini ukawa mbaya zaidi baina ya pande hizo mbili tangu baada ya kusambaratika Urusi ya zamani."

Kwa msingi huo serikali ya Biden imetanguliza mbele siasa za kukabiliana na Russia; na mbali na kuiwekea vikwazo mtawalia na kuwaunga mkono mahasimu na wapinzani wa Moscow kama Ukraine, Marekani imeanzisha vita kali ya kinafsi dhidi ya Rais Vladimir Putin mwenyewe.

Katika mazingira haya ya mvutano mkubwa katika uhusiano wa Washington na Moscow hakuna matarajio ya kupatikana matunda ya maana katika mazungumzo ya Biden na Putin.

Pamoja na hayo na kwa kuzingatia ukuruba wa misimamo ya Ulaya na Marekani baada ya kipindi cha Trump, inatazamiwa kuwa safari ya Biden barani Ulaya itazidisha mshikamano na umoja baina ya nchi hizo dhidi ya Russia.

Tags